UTURUKI
1 dk kusoma
Trump, Erdogan waahidi ushirikiano wa karibu zaidi, waangazia mauzo ya ndege za kivita na biashara
Trump amempongeza rais wa Uturuki akimtaja kuwa "mtu anayeheshimika sana", akisema kuwa Erdogan anapendwa "sana katika nchi yake na kote barani Ulaya, na duniani kote".
Trump, Erdogan waahidi ushirikiano wa karibu zaidi, waangazia mauzo ya ndege za kivita na biashara
Trump anasema yeye na Erdogan watajadili kuhusu manunuzi ya Uturuki ya ndege za kivita za Marekani, ikiwemo F-16 na F-35. / AP
25 Septemba 2025

Rais wa Marekani Donald Trump na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan wameapa kuimarisha ushirikiano kuhusu masuala ya ulinzi na biashara wakati wa mazungumzo yao katika Ikulu ya Marekani ya White House siku ya Alhamisi.

Trump amesema kuwa yeye na Erdogan watajadili kuhusu Uturuki kununua ndege za kivita zilizotengenezwa Marekani, ikiwemo F-16 na F-35, pamoja na ushirikiano wa kiuchumi.

“Tutatia saini makubaliano muhimu kwa nchi zetu zote mbili,” Trump aliwaambia waandishi wa habari, akiongeza kuwa vikwazo kwa Uturuki kuhusu kununua mifumo ya makombora kutoka kwa Urusi huenda vikaondolewa “mara moja”.

Akiwa amekaa pembeni mwa Trump katika ofisi ya rais ya Oval, Erdogan alisema majadiliano yataangazia masuala mbalimbali, ikiwemo mauzo ya ulinzi.

“Tuko katika mchakato tofauti wa uhusiano wa Uturuki na Marekani,” alisema. “Naamini kwa pamoja, mkono kwa mkono, tutaweza kukabiliana na hizi changamoto katika kanda.”

Trump alimpongeza mwenzake kuwa “mtu ambaye anaheshimika sana”, akisema Erdogan anapendwa “sana nchini kwake na kote barani Ulaya, na duniani kote”.

Mkutano huu unakuja baada ya tofauti za muda mrefu kujitokeza kati ya washirika wa NATO kuhusu manunuzi ya kijeshi, mapigano katika kanda na vikwazo vya kifedha, lakini viongozi wote walionekana kufikia muafaka, na kusisitiza ushirikiano kuliko makabiliano.

CHANZO:TRT World