Timu ya soka ya Kenya imefuzu kwa hatua ya makundi ya mashindano ya Shirikisho barani Afrika, CAF baada ya kuifunga Etoile Sportive du Sahel ya Tunisia 7-6 kupitia penati.
Matokeo ya jumla baada ya kucheza mechi zote mbili yalikuwa sare ya 2-2 na kulazimisha mechi hiyo kuamuliwa kwa penati.
Nairobi United ilipata ushindi wake wa 2-0 mjini Nairobi wiki mbili zilizopita na Etoile du Sahel wakalipiza kisasi kwa tofauti hiyo katika uwanja wao wa nyumbani nchini Tunisia.
Nyota wa mechi hiyo alikuwa golikipa wa United, Kevin Oduor ambaye aliokoa penati ya saba ya Etoile, kabla ya yeye mwenyewe kufunga ya kwake, na kuweka historia ya kuingia hatua ya makundi ya kombe la Shirkisho kwa mara ya kwanza.
Timu hiyo ya kandanda inayojulikana kama Naibois ilifika hatua hii baada ya ubingwa wake wa ligi daraja la pili nchini Kenya msimu uliopita, hatua iliyowafanya pia wapandishwe daraja hadi kwenye Ligi Kuu ya nchini humo.










