Rais wa Malawi Arthur Peter Mutharika ametangaza hali ya janga la kitaifa katika wilaya kumi na moja za nchi zinazokabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula kutokana na kiangazi cha muda mrefu.
Justin Saidi, Katibu Mkuu wa Rais, alitoa taarifa Jumamosi, akisema Rais Mutharika "ameeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu matatizo ya ukosefu wa chakula kutokana na athari za kiangazi cha muda mrefu."
Kulingana na Ripoti ya hivi majuzi ya Hali ya Chakula kutoka Kamati ya Tathmini ya Mazingira Hatarishi ya Malawi (MVAC), takriban watu milioni 4 wako katika hatari ya kukumbwa na uhaba mkubwa wa chakula mwaka huu na mapema mwaka ujao.
"Rais kwa hiyo anaomba msaada wa ndani na wa kimataifa kwa familia zilizoathirika. Idadi ya watu walioathiriwa na kiangazi ni kubwa sana. Kwa hiyo hebu tusaidie jamii zilizoathirika haraka iwezekanavyo," Saidi alisema.
Wilaya zilizoathiriwa ziko katika mikoa minne ya kiutawala nchini.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Malawi imepitia vipindi vya mabadiliko ya tabianchi vilivyosababishwa na El Nino, ambavyo vimeathiri upatikanaji wa chakula.














