Waziri Mkuu wa Tanzania, Mwigulu Nchemba amewataka Watanzania watunze akiba ya chakula walichonacho na waepuke matumizi yasiyofaa kutokana na hali ya kuchelewa kwa msimu wa mvua.
Akizungumza na baadhi ya Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya, ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma, Nchemba alisema kuwa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa utabiri wa mwelekeo wa msimu wa mvua za vuli na mvua za msimu kwa kipindi cha Oktoba 2025 hadi Disemba 2025 na kipindi cha mwezi Novemba, 2025 hadi Aprili 2026 mtawalia.
“Kutokana na utabiri huo, baadhi ya mikoa nchini inatarajiwa kuwa na mvua za chini ya wastani hadi wastani na kutawaliwa na vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko wa mvua usioridhisha,” amesema.
Kulingana na Nchemba, TMA ilionesha hali ya kuchelewa kwa mvua inatarajiwa katika maeneo ya mikoa ya Dodoma, Katavi, Kigoma, Singida, Tabora, Iringa, Mbeya, Mtwara, Njombe, Songwe, Rukwa, Ruvuma pamoja na Kusini mwa Mkoa wa Morogoro.
“Pamoja na kuwa hakuna tishio la uhaba wa chakula kutokana na hifadhi ya chakula iliyopo nchini, lakini ni vema, wananchi waendelee kuzingatia matumizi sahihi ya chakula. Tuna akiba ya chakula ya kutosha lakini ninawasihi wananchi waweke akiba na kuepuka matumizi yasiyo ya lazima,” alisisitiza.
Kiongozi huyo alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wakulima nchini Tanzania, kuandaa mashamba kwa wakati na watumie pembejeo zinazoendana na upatikanaji wa mvua chache sanjari na kuzingatia ushauri wa wataalamu wa kilimo ambao kwa sasa wanazunguka nchi nzima kukutana na wakulima, wakitoa elimu.
















