Luteni Jenerali Fanil Sarvarov, afisa wa juu wa kijeshi, alifariki dunia baada ya kilipuzi kulipuka chini ya gari lake asubuhi ya Jumatatu, kwa mujibu wa Kamati ya Uchunguzi ya Urusi.
Katika taarifa iliyotolewa kupitia jukwaa la mawasiliano la Telegram, kamati hiyo ilisema kuwa Luteni Jenerali Sarvarov, ambaye alikuwa mkuu wa Idara ya Mafunzo ya Kiutendaji ya Makao Makuu ya Jeshi la Urusi, alikufa kutokana na majeraha yaliyosababishwa na mlipuko huo.
“Kwa mujibu wa wachunguzi, asubuhi ya Desemba 22, kilupizi kilichokuwa kimetegwa chini ya gari kililipuliwa katika Mtaa wa Yasenevaya jijini Moscow,” ilisema taarifa hiyo.
Kamati hiyo iliongeza kuwa uchunguzi umeanzishwa rasmi kufuatia kufunguliwa kwa kesi ya jinai mjini Moscow. Wachunguzi wanasema wanaendelea kuchunguza nadharia mbalimbali kuhusu mauaji hayo, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kuhusika kwa idara za kijasusi za Ukraine.
Hadi sasa, mamlaka za Ukraine bado hazijatoa ufafanuzi wowote kuhusu madai hayo.













