Serikali ya Venezuela imewaachilia huru watu 88 waliokamatwa kufuatia maandamano ya baada ya uchaguzi wa nchi hiyo uliofanyika Julai 2024.
Hii ni mara ya pili kwa idadi kubwa ya watu kuachiliwa katika kipindi cha wiki mbili huku shinikizo kutoka Marekani likizidi kuongezeka.
Kuachiliwa siku ya Mwaka Mpya kunafuata tangazo la serikali kwamba watu 99 waliachiliwa Disemba 26, na kufanya idadi ya walioachiwa katika kipindi hicho kufikia 187.
Serikali ilisema katika taarifa: "Hatua hizi ni sehemu ya mchakato wa ukaguzi wa kina wa kesi uliotolewa na Rais Nicolas Maduro."
Kamati ya Uhuru wa Wafungwa wa Kisiasa, shirika lisilo la kiserikali la Venezuela, ilisema kwamba imehakiki kuachiliwa kwa takriban wafungwa 55, isipokuwa mmoja kutoka gereza la Tocoron katikati ya Venezuela.
Baada ya tangazo la Disemba 26, vikundi kadhaa vya kutetea haki za binadamu vilidai kutoamini iwapo idadi ya wafungwa waliotolewa ndio idadi rasmi ya wafungwa.
Mvutano
Kuachiliwa kwa wafungwa hao kunatokana na shinikizo kutoka kwa utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye amesema itakuwa "busara" kwa Maduro kuondoka madarakani.
Marekani hivi karibuni imeongeza uwepo wake wa kijeshi katika eneo la Karibiani, na kushambulia meli karibu na pwani ya Venezuela ambazo inadai zilihusika katika usafirishaji wa madawa ya kulevya, na kukamata meli mbili za mafuta ghafi ya Venezuela.
Serikali ya Venezuela imelaani mara kwa mara vitendo vya Marekani, ikisema Marekani inaingilia mambo ya ndani na kuendesha vita vya kiuchumi.




















