Uwanja wa Ndege wa Sabiha Gökçen, ambao ni kituo cha usafiri wa anga upande wa Asia wa jiji la Istanbul, ulihudumia abiria milioni 44.2 kati ya Januari na Novemba, na kuvunja rekodi ya mwaka uliopita ya abiria milioni 41.4.
Waziri wa Uchukuzi na Miundombinu wa Uturuki, Abdulkadir Uraloğlu, alisema Alhamisi kuwa njia mpya ya ndege, iliyofunguliwa Desemba 2023 ili kuruhusu ndege kubwa kutua, imechangia kwa kiasi kikubwa kufikiwa kwa rekodi hiyo.
Taarifa hiyo ilitolewa katika maadhimisho ya miaka miwili tangu njia hiyo mpya ya ndege ianze kufanya kazi.
Uraloğlu alisema kuwa, pamoja na njia hiyo mpya, miundombinu mingine kama njia za kupitisha ndege (taxiway), maeneo ya maegesho ya ndege zenye uwezo mkubwa na mizigo, mnara wa kudhibiti safari za ndege, pamoja na majengo ya kisasa, vimeongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa uwanja wa ndege wa Sabiha Gökçen kuhudumia safari za anga.
Mwaka 2023, jumla ya abiria milioni 33.7 walihudumiwa kwenye safari za ndani na za kimataifa kati ya Januari na Novemba.
“Idadi ya abiria iliongezeka kwa asilimia 31 katika miezi 11 ya mwaka 2025 ikilinganishwa na kipindi cha kabla ya njia ya pili ya ndege kuanza kufanya kazi mwaka 2023,” alisema.
“Ndani ya miezi 11 pekee, tulipita rekodi ya abiria milioni 41.4 iliyofikiwa katika mwaka mzima wa 2024,” aliongeza.
Uraloğlu pia alisema kulikuwa na safari za ndege 208,643 kati ya Januari na Novemba 2023, na idadi hiyo ikaongezeka kwa asilimia 20 hadi kufikia 250,538 katika kipindi hicho hicho mwaka huu. Aliongeza kuwa, “Kwa mwaka mzima wa 2024, idadi hiyo ilikuwa ndege 242,612.”



























