Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON 2025 yanayoendelea nchini Morocco, si tu yameunganisha mamilioni ya mashabiki wa soka, bali pia yamefungua milango mipya ya fursa za biashara kwa wasanii na wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika.
Katika maeneo maalum kama Fan Zone na maeneo ya mikusanyiko ya mashabiki, wasanii wanapata nafasi ya kuonyesha kazi zao kwa hadhira pana ya kimataifa.
Miongoni mwao ni Agnes Mpata, mchoraji wa sanaa ya Tingatinga kutoka Tanzania, ambaye kwa sasa anaonesha kazi zake mjini Rabat.
“Mimi ni mchoraji wa sanaa ya Tanzania inayoitwa Tingatinga Arts, kutoka Dar es Salaam,” anasema Agnes.
Anafafanua kuwa aliletwa Morocco na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA), lililo chini ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, ili kushiriki maonesho sambamba na mashindano ya AFCON.
Kwa Agnes, AFCON imekuwa zaidi ya tukio la michezo.
“Ni fursa adimu kuja kuonesha kazi zako nje ya nchi. Naishukuru sana serikali yangu kwa kunipa nafasi hii,” aliiambia TRT Afrika.
Anaeleza kuwa biashara imekuwa nzuri hasa siku ambazo timu kubwa kama Morocco zinapocheza, kwani idadi ya mashabiki huongezeka kwa kiasi kikubwa.
“Siku ambazo Morocco inacheza, watu wanakuwa wengi sana mpaka tunachanganyikiwa,” anasema kwa tabasamu. Hata hivyo, anakiri kuwa siku ambazo hakuna mechi kubwa, biashara hupungua kidogo.
Kupitia uzoefu wake, Agnes amejifunza umuhimu wa kuielewa soko la mwenyeji. Anasema kuwa aligundua mashabiki wa Morocco wanapenda sana michoro ya simba, jambo lililomsaidia kubadilisha mkakati wake wa biashara.
“Nitaandaa michoro ambayo wao wataipendelea,” anasema.
AFCON 2025 imeonesha kwa vitendo jinsi michezo mikubwa inavyoweza kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kitamaduni.
Mbali na kuleta msisimko wa soka, mashindano haya yamekuwa jukwaa la kujitangaza, kubadilishana tamaduni na kukuza biashara za Waafrika.
“Wasanii wasihofu kushiriki matamasha kama haya,” anashauri Agnes.“
Ni fursa ya kujitangaza, kuitangaza kazi yako na pia kuitangaza nchi yako.
Kwa wengi, AFCON 2025 nchini Morocco imekuwa ushahidi kwamba soka linaweza kuunganisha Afrika, si tu kupitia ushindi uwanjani, bali pia kupitia fursa za maisha nje ya viwanja.














