| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Waziri Mkuu wa Tanzania awaonya wasio na dharura kutotoka nje siku ya Disemba 9
Waziri Mkuu wa Tanzania Mwigulu Nchemba amewataka Watanzania kuitumia Disemba 9 ambayo ni Siku ya Uhuru wa Tanzania Bara kama siku ya mapumziko wakiwa majumbani mwao.
Waziri Mkuu wa Tanzania awaonya wasio na dharura kutotoka nje siku ya Disemba 9
Onyo wa Waziri Mkuu wa Tanzania Mwigulu Nchemba unakuja kufuatia hofu ya kuwa na maandamano Disemba 9. / / Reuters
8 Desemba 2025

Akiongea kwa niaba ya Rais wa nchi hiyo Samia Suluhu Hassan, Mwigulu amesema wanaotakiwa kuwepo kazini ni wale tu ambao majukumu yao yanawataka wawepo katika vituo vya kazi.

“Serikali inawashauri wananchi wote, ambao tarehe 9 Disemba, 2025, hawatakua na dharura kuitumia siku hiyo kwa mapumziko, hivyo kusherehekea siku hiyo wakiwa nyumbani, isipokuwa kwa wale ambao majukumu yao ya kazi yanawataka kuwepo katika vituo vyao vya kazi, kama ambavyo wataelekezwa na viongozi wao”. Waziri huyo amesema.

Kauli hii inakuja wakati ambao, tayari nchini humo kuna vuguvugu ya baadhi ya wananchi kutaka kufanya maandamano ya kudai mabadiliko ya kiutawala nchini humo. Hata hivyo, polisi tayari imeyapiga marufuku maandamano hayo na kusema sio halali.

Hali hiyo ya wasiwasi nchini humo, inaripotiwa kuzua taharuki miongoni mwa mwananchi, hasa katika miji mikubwa kama Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Arusha na hata Mbeya, ambapo siku mbili hizi kumeshuhudiwa idadi kubwa ya watu wanaonunua bidhaa mbalimbali kwa ajili ya kuweka ndani, huku wakihofia kutokea kwa vurugu kama za Oktoba 29 baada ya uchaguzi.

Wakati huo huo, Mufti wa Tanzania Abubakar Zubeir, amewataka Waislamu wa nchi hiyo, na waumini wa dini nyengine kutojihusisha na maandamano hayo yaliyopangwa kufanyika Siku ya Uhuru.

Tayari taifa hilo la Afrika Mashariki, ambalo kwa miaka yote lina sifa ya utulivu wa kisiasa, kwa kiasi fulani limegubikwa na hali ya wasiwasi, huku mpasuko mkubwa wa maoni na fikra ukishuhudiwa miongoni mwa wananchi.

CHANZO:TRT Afrika