Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Felix Tshisekedi ameituhumu Rwanda kwa kwenda kinyume na makubaliano ya amani kati ya nchi hizo mbili, yaliyotiwa saini nchini Marekani, hivi karibuni.
Kulingana na Tshisekedi, siku moja baada ya kusainiwa kwa mkataba huo wa amani, Rwanda iliishambulia DRC kutoka mji wa Bugarama na kusababisha uharibifu mkubwa katika maeneo ya Kaziba, Katogota na Lubarika yaliyoko Kusini mwa Kivu.
"Rwanda imeanza kukiuka makubaliano hayo,” alisema Tshisekedi wakati akilihutubua bunge la nchi hiyo siku ya Jumatatu.
Hata hivyo, Rwanda imekana tuhuma za DRC, na kuyaita kuwa ni ‘kichekesho’.
Disemba 4, 2025, wawili hao walitia saini mkataba wa ‘kihistoria’ mbele ya Rais Donald Trump wa Marekani, kwa lengo la kumaliza machafuko katika eneo la Mashariki mwa DRC.














