UTURUKI
3 dk kusoma
Uturuki kuandaa mazungumzo ya Gaza wiki ijayo kufuatia wasiwasi juu ya usitishaji mapigano – Fidan
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, amesema kuwa Ankara imechukua jukumu muhimu chini ya Azimio la Sharm el-Sheikh, ikishirikiana na washirika wa kimataifa kuhakikisha kuwa usitishaji wa mapigano huko Gaza unakuwa wa kudumu.
Uturuki kuandaa mazungumzo ya Gaza wiki ijayo kufuatia wasiwasi juu ya usitishaji mapigano – Fidan
Tsahkna aliipongeza Uturuki kwa Siku ya Jamhuri ya nchi hiyo, akisisitiza kwamba Uturuki inasalia kuwa mshirika muhimu na dhabiti wa Estonia. / / AA
31 Oktoba 2025

Waziri wa Mambo ya Njew wa Uturuki, Hakan Fidan, amesema siku ya Ijumaa ya kwamba mawaziri wa mambo ya nje kutoka baadhi ya nchi za Kiislamu watakutana Istanbul siku ya Jumatatu kujadili hali ya usitishaji wa mapigano huko Gaza na hatua zinazofuata, huku akionyesha wasiwasi kuhusu kama usitishaji huo utaendelea.

Akizungumza katika mkutano wa wanahabari mjini Ankara, Uturuki, Fidan ameeleza kuwa mkutano huo utawakutanisha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi ambazo zilihudhuria kikao na Rais wa Marekani, Donald Trump, mjini New York mwezi Septemba.

Mkutano huo uliolenga kujadili hali ya Gaza ulihudhuriwa na Uturuki, Qatar, Saudi Arabia, Misri, Falme za Kiarabu (UAE), Jordan, Pakistan na Indonesia.

Fidan amesema: “Mada zinazojadiliwa sasa ni jinsi ya kusonga mbele kuelekea awamu ya pili – yaani kikosi cha kudumisha uthabiti.”

Waziri, akiashiria ukiukaji wa makubaliano wa usitishaji vita kwa upande wa Israel. Fidan amesema: “Ni wazi Netanyahu anatafuta visingizio vya kuvunja mkataba wa usitishaji wa mapigano na kuanzisha tena mauaji ya halaiki mbele ya macho ya dunia nzima. Ni jambo dhahiri. Kwa ajili ya kuhifadhi matumaini ya amani ya kudumu na kuhakikisha usalama wa eneo hili, Israel lazima izingatie masharti ya usitishaji mapigano.”

Fidan aliongeza kuwa kupitia Azimio la Sharm el-Sheikh, Uturuki imechukua jukumu muhimu na inafanya kazi kwa karibu na nchi husika kuhakikisha usitishaji mapigano unakuwa wa kudumu.

Alisisitiza umuhimu wa jumuiya ya kimataifa kupeleka ujumbe unaofaa kwa Israel. “Misaada yetu ya kibinadamu kwa Gaza inaendelea bila kusita. Maafisa kutoka Wizara yetu ya Afya, AFAD na Shirika la Hilali Nyekundu wa Uturuki wanaendeleza shughuli za misaada mjini Rafah. Meli yetu ya misaada yenye tani 900 ilifika katika bandari ya Al Arish, Misri, tarehe 17 Oktoba, na maandalizi ya misheni ya huduma za kibinadamu, Mungu akipenda, yatakamilika hivi karibuni,” alisema Fidan.

Aliongeza kuwa Uturuki imeandaa kila liwezekanalo ili kuwaleta ndugu zao Wapalestina nchini humo kwa ajili ya matibabu.

“Tutaendelea kufanya kila tuwezalo kusaidia ujenzi upya wa Gaza, na tunaamini kuwa kwa uvumilivu na mshikamano, Gaza itainuka tena,” alisema.

Inayohusiana

“Uturuki inasalia kuwa mshirika muhimu na imara kwa Estonia”

Katika mkutano huo huo wa wanahabari baada ya mazungumzo yake na Fidan, Waziri wa Mambo ya Nje wa Estonia, Margus Tsahkna, amesema kuwa “hali ya kibinadamu huko Gaza ni ya kusikitisha sana,” akiongeza kuwa “ni lazima shinikizo kubwa liwekwe dhidi Israel.”

Akiashiria mchakato wa usitishaji mapigano na kuachiliwa kwa wafungwa unaoendelea Gaza, Tsahkna alisema kuwa Estonia imekuwa ikiiunga mkono mara kwa mara suluhisho la mataifa mawili, na kwamba Tallinn inaunga mkono maazimio ya Umoja wa Mataifa kuhusu Palestina na pia ni sehemu ya Azimio la New York.

Tsahkna amesisitiza kuwa Estonia inaendelea kutoa misaada ya kibinadamu kwa Gaza kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) na mashirika mengine.

Ameongeza kuwa ili kuendeleza juhudi za amani huko Gaza, ni muhimu pia mataifa mengine zaidi tofauti na Uturuki, yaendelee kuweka shinikizo.

Aidha, Tsahkna aliipongeza Uturuki kwa Siku ya Jamhuri, akisisitiza kuwa Uturuki inaendelea kuwa mshirika muhimu na mwenye nguvu kwa Estonia, na kwamba uhusiano wa pande mbili unakua kwa kasi.

Kwa upande wake, Fidan amesema mazungumzo yake na waziri wa Estonia yameimarisha zaidi dhamira ya pamoja ya mataifa hayo kuendeleza ushirikiano na urafiki, na kwamba wamejadili pia ushirikiano ndani ya NATO, usalama wa Euro-Atlantiki, na mchakato wa Uturuki wa kujiunga na Umoja wa Ulaya (EU).

CHANZO:TRT World and Agencies