Mapigano mapya kati ya waasi wa M23 na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) yalizuka siku ya Jumanne, katika maeneo tofauti ya Mashariki mwa DRC.
Mapigano hayo yalizuka asubuhi ya Jumanne katika maeneo ya Walungu na Uvira, huko kusini mwa jimbo la Kivu, na kutatiza masomo na biashara.
Baadhi ya wakulima waliokuwa mashambani mwao, waliripotiwa kutafuta maeneo ya usalama, baada ya mapigano hayo kuzidi kuongezeka kwenye eneo la Kamanyola.
Katika taarifa yake kuhusu mapigano hayo, Jeshi la Ulinzi la nchini DRC (FARDC), limeituhumu Rwanda kwa kushirikiana na kikundi cha waasi wa M23 kwa kuratibu mfululizo wa mashambulizi katika maeneo ya Kaziba, Katogota na Lubarika.
Hivi karibuni, serikali ya DRC na kikundi cha M23 zilitiliana saini mkataba wa amani jijini Doha, ukisimamiwa na Qatar.












