Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amekutana na Sultan Haitham bin Tariq wa Oman mjini Muscat siku ya Alhamisi kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano wa pande mbili katika nyanja za viwanda, ulinzi, na mawasiliano.
Viongozi hao wamejadili masuala ya kikanda na ya kimataifa, wakithibitisha msimamo wao wa pamoja kuhusu kadhia ya Palestina. Ziara hii ilikuwa hatua ya mwisho ya ziara ya Erdogan katika nchi tatu za Ghuba, baada ya kuzuru Kuwait na Qatar.
Kikao hicho kimefanyika katika Kasri ya Al Alam jijini Muscat, mji mkuu wa Oman, katika mkutano wa faragha, kwa mujibu wa vyanzo vya kidiplomasia vya Uturuki.
Taarifa iliyotolewa na Idara ya Mawasiliano ya Uturuki ilisema kuwa viongozi hao walijadili uhusiano wa mataifa mawili pamoja na masuala ya kikanda na kimataifa.
“Rais Erdogan alieleza kuwa Uturuki na Oman zina uhusiano wa kihistoria na kindugu wa muda mrefu, na kwamba ziara hii imeimarisha zaidi mshikamano kati ya mataifa haya mawili,” ilisema taarifa hiyo.
“Akitilia mkazo kuwa Uturuki na Oman zina misimamo sawa katika masuala mengi, hususan suala la Palestina, Rais Erdogan alitoa pongezi kwa juhudi za Oman katika eneo hilo kupitia upatanishi na mazungumzo, na akaongeza kuwa kutakuwa na juhudi za pamoja kufanikisha suluhisho la mataifa mawili kwa tatizo la Gaza,” ilisema taarifa hiyo.
Baada ya mkutano huo, nyaraka mpya 16 zilisainiwa kati ya nchi hizo mbili, kwa mujibu wa Idara ya Mawasiliano ya Uturuki.


















