Kiongozi wa upinzani wa Cameroon, Anicet Ekane, aliyekamatwa mwezi Oktoba kwa mashtaka ya uasi, alifariki Jumanne akiwa kizuizini, alisema wakili wake. Alikuwa na umri wa miaka 74.
Wakili Emmanuel Simh aliwaambia waandishi wa habari kuwa Ekane amekuwa akezuiliwa katika makao ya gendarmarie tangu alipokamatwa tarehe 24 Oktoba kwa mashtaka ya uasi.
Simh alidai kuwa Ekane alikuwa "mgonjwa akiwa katika hali hatari, lakini hakupata matibabu yanayostahili" wakati alikuwa mahabusu.
Wizara ya Ulinzi ya Cameroon ilisema marehemu alikuwa na magonjwa sugu na alipata "huduma stahiki kutoka kwa Jeshi la Tiba la Kijeshi," kwa ushauriano na madaktari wake binafsi.
Uchunguzi umezinduliwa ili kubainisha chanzo cha kifo
"Marehemu, ambaye alikuwa na magonjwa mbalimbali sugu, alikuwa amelazwa hospitalini katika Kituo cha Tiba cha Taifa cha Gendarmarie," ilisomewa katika taarifa ya wizara.
Wizara ilisema uchunguzi ulianzishwa ili kubaini hali halisi zilizopelekea kifo cha Ekane.
Ekane, aliyekuwa kiongozi wa Harakati ya Afrika kwa Uhuru Mpya na Demokrasia (MANIDEM), alikamatwa pamoja na viongozi wengine wakuu wa upinzani katikati ya maandamano yaliyotikisa nchi kutokana na madai ya ulaghai katika uchaguzi wa urais wa karibuni.
Kukamatwa huko Douala, mji wa kibiashara wa Cameroon, kulitokea baada ya kutangaza kuunga mkono Issa Tchiroma Bakary, aliyekuwa mpinzani wa Rais Paul Biya katika uchaguzi wa urais wa tarehe 12 Oktoba.
Rais Biya apata tena uteuzi
Biya, mwenye umri wa miaka 92, alitangazwa mshindi wa uchaguzi, ambao Tchiroma alidai yeye ndiye aliyeshinda.
Mwezi uliopita, Tchiroma alitafuta hifadhi nchini The Gambia, akieleza wasiwasi juu ya usalama wake kufuatia mvutano wa kisiasa wa hivi karibuni.













