Uturuki inaendelea kukuza amani na mazungumzo, Rais Recep Tayyip Erdogan alisema Ijumaa katika jukwaa la kimataifa nchini Turkmenistan.
Akizungumza katika Jukwaa la Amani na Kuaminiana mjini Ashgabat, Erdogan alisema Ankara inafanya kazi “kwa nguvu zetu zote” kuhakikisha diplomasia inashinda, ikiegemea historia, jiografia na wajibu wa kitamaduni wa nchi hiyo.
“Kwa upande wa Uturuki, tunafanya kazi kwa nguvu zetu zote—tukiongozwa na hisia za uwajibikaji zinazotokana na historia, jiografia na ustaarabu wetu—ili kuhakikisha kuwa amani na mazungumzo zinatawala,” Erdogan alisema.
Aliongeza pia kuwa Uturuki iko tayari kuunga mkono juhudi za kidiplomasia za kuhakikisha usitishwaji wa vita na amani ya kudumu, ikijumuisha juhudi zinazohusiana na mgogoro wa Urusi na Ukraine.
Kuhusu Mashariki ya Kati, Erdogan alisisitiza kuwa mchakato wowote wa amani ni lazima umshirikishe Mpalestina na hatimaye kupelekea suluhisho la mataifa mawili.
Alionya pia kuwa usitishwaji mapigano wa Oktoba kati ya Israel na Hamas huko Gaza bado ni dhaifu, na akatoa wito wa kuendelezwa kwa msaada wa kimataifa ili kuudumisha.
Turkmenistan nchi isiyoegemea upande wowote
Rais Erdogan alihudhuria hafla ya kuweka shada la maua katika mnara wa “Neutrality Monument”, huku viongozi wa dunia wakikusanyika mjini Ashgabat
Erdogan alijiunga na viongozi kadhaa wa nchi na serikali walioalikwa katika hafla hiyo, akiwamo Rais wa Urusi Vladimir Putin na Rais wa Iran Masoud Pezeshkian.
Baadaye Erdogan alishiriki katika picha ya pamoja baada ya sherehe rasmi ya mapokezi katika ukumbi wa jukwaa hilo.
Viongozi hao wanatarajiwa kuhudhuria kikao cha ufunguzi cha mkutano huo baadaye leo.
Jukwaa hilo mjini Ashgabat linafanyika kuadhimisha miaka 30 ya hadhi ya Turkmenistan kama nchi yenye upande usioegemea upande wowote, pamoja na tamko la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililotangaza mwaka 2025 kuwa “Mwaka wa Kimataifa wa Amani na Kuaminiana.”

















