Katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Prince Moulay Abdallah Mjini Rabat, mashabiki zaidi ya 60,000 walijaa uwanjani kushuhudia mtanange huo wa kukata na shoka.
Kipindi cha kwanza: Udi na uvumba goli lazima lipatikane
Wakati huo kila timu ikipambana kusaka bao, mlinzi wa kati wa Cameroon nambari 2 mgongoni Junior Baptiste alipata majeraha na nafasi yake kuchukuliwa na kiungo mkabaji Eric-Junior Ebimbe mnamo dakika ya 24 ya mchezo.
Mnamo dakika ya 27 Brahim Diaz akaitanguliza Morocco baada ya kusukumiza wavuni pasi ya kichwa kutoka kwa Ayoub El Kaabi aliyepokea mpira wa kona.
Baada ya bao hilo la kuongoza kwa vijana wa kocha Walid Regragui, patashika za mtanange huu ziliendelea na mashambulizi kupamba moto, lakini safu za washambuliaji hazikuwa makini vyakutosha.
Mlinda lango la Morocco Yassine Bounou ni kama alitulia zaidi golini mwake bila kupata kashkashi za kuhatarisha.
Lakini mwenzake wa Cameroon, Devis Epassy alikuwa na wakati mgumu wa kuokoa ‘michomo’ iliyokuwa ikielekezwa langoni mwake.
Kindi cha kwanza kiliisha huku ‘Simba wa milima ya Atlas’ wakiongoza bao moja kwa nunge.
Kipindi cha pili: Matumaini dhidi ya ujasiri
Kwa ujasiri mkubwa wakibebwa na historia ya ubingwa wa AFCON, Cameroon walianza kipindi cha pili kwa mashambulizi ya kushtukiza, japo safu ya ulinzi ya Morocco ilikuwa makini kudhibiti mashambulizi hayo.
Timu zote zilishambuliana kwa zamu na hasa baada ya kujua mbinu za kila mpinzani mchezo ulionekana kuwa si rahisi.
Na hatimaye dakika ya 74 Ismael Saibari akapachika bao la pili kwa mkwaju mkali ndani ya kumi na nane na kufanya matumaini ya Morocco kutinga nusu fainali ya AFCON 2025 kukamilika.
Dakika 90 zilimalizika kwa ushindi kwa Morocco ya akina Achraf Hakiki na wenzake, baada ya kuibugiza Cameroon goli mbili kwa mtungi.
Sasa Wamorocco wanasubiria kumjua mpinzani wao wa kucheza naye nusu fainali kati ya Algeria au Nigeria ambao wana pambano litakalopigwa hapo tarehe 10 Januari 2026 katika mji wa buluu wa Marrakesh.



















