Wakenya wamejitokeza kwa wingi kuomboleza kifo cha Odinga tangu alipoaga dunia Jumatano, jambo linaloonyesha ushawishi mkubwa wa kiongozi huyo aliyeheshimiwa katika siasa za nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Msongamano ulitokea katika uwanja huo uliopo jijini Nairobi, wakati umma ulipokuwa ukiuaga mwili wa Odinga.
Shirika la Msalaba Mwekundu wa Kenya limesema tukio hilo "lilisababisha watu wengi kuhitaji huduma za dharura." Chanzo katika hospitali kuu ya rufaa nchini kilisema walipokea watu 18 waliokuwa wamejeruhiwa.
Maelfu ya watu wamejaza uwanja wa Nyayo ambapo jeneza la Odinga lilifunikwa na bendera ya taifa kwa ajili ya ibada ya Kanisa la Anglican. Watu walikuwa wakimwimbia nyimbo na kuonyesha picha za Odinga, huku wengine wakibeba matawi, ambayo ni ishara ya amani na mshikamano katika mila za Kenya.
Kulikuwa na usalama mkali uwanjani baada ya watu wanne kuripotiwa kufariki dunia wakati wa kuuaga mwili wa Odinga siku ya Alhamisi, wakati polisi walipojaribu kudhibiti umati mkubwa katika uwanja Kasarani.
Angalau watu 10 walijeruhiwa katika tukio la Alhamisi baada ya polisi kufyatua risasi na kutumia mabomu ya machozi dhidi ya umati uliokuwa ukijaribu kufikia eneo la jeneza.