Rais wa Marekani Donald Trump ameonya kuhusu "hatua kali zaidi" iwapo mamlaka nchini Iran zitaendelea kuwatisha baadhi ya waandamanaji kuwa itawaua, huku Iran ikitaja onyo hilo la Marekani kuwa "kisingizio cha kushambulia kijeshi".
Trump — ambaye awali aliwaambia waandamanaji nchini Iran kuwa "anawaletea msaada" — alisema siku ya Jumanne katika mahojiano ya shirika la CBS kuwa Marekani itachukua hatua iwapo Iran itaanza kuwanyonga waandamanaji.
Waendesha mashtaka wa Iran wamesema kuwa mamlaka nchini humo zitawasilisha mashtaka ya "moharebeh", au "vita dhidi ya Mungu", kwa baadhi ya washukiwa waliokamatwa katika maandamano ya hivi karibuni.
"Tutachukua hatua kali iwapo watafanya hivyo," alisema rais huyo wa Marekani, ambaye mara kwa mara amekuwa akitishia Iran na mashambulizi ya kijeshi.
"Wanapoanza kuwaua maelfu ya watu — na sasa unaniambia kuhusu kuwanyonga. Tutaona vile itakavyokuwa kwao," Trump alisema.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani katika mtandao wa X wa lugha ya Kifarsi ilisema muandamanaji mwenye umri wa miaka 26 Erfan Soltani amehukumiwa kuuawa siku ya Jumatano.
"Erfan ni muandamanaji wa kwanza kuhukumiwa kifo, lakini hatokuwa wa mwisho," Wizara ya Mambo ya Nje imesema, ikiongeza kuwa raia wa Iran zaidi ya 10,600 wamekamatwa.
‘Lengo ni kubadilisha utawala ’
Wakati huohuo Ujumbe wa Iran katika Umoja wa Mataifa, umeweka taarifa kwenye mtandao wa X, ukiapa kuwa "njama hiyo" ya Marekani "haitofanikiwa tena".
"Fikra za Marekani na sera zake kwa Iran zinalenga kubadilisha utawala, vikwazo, vitisho, kusababisha vurugu, ili kutengeneza kisingizio cha mashambulizi ya kijeshi," ujumbe ulisema.
Shirika la habari la taifa la Iran limesema kuwa maafisa kadhaa wa usalama wameuawa, huku mazishi yakigeuzwa kuwa maandamano makubwa ya kuunga mkono serikali.
Mamlaka nchini humo zimetangaza mazishi makubwa katika mji mkuu Tehran siku ya Jumatano kwa "mashahidi" wa siku za hivi karibuni.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanashtumu serikali kwa kuwafyatulia risasi waandamanaji na kuficha ukubwa wa tatizo hilo huku mtandao ukizimwa ambapo imepita zaidi ya siku tano sasa.
Mamlaka nchini Iran zimesisitiza kuwa zimefanikiwa kudhibiti nchi tena baada ya siku kadhaa za maandamano mfululizo kote nchini.


















