Wapiganaji nchini Sudan wa kundi la RSF wamekuwa wakifanya kwa makusudi maujai ya kikatili na kuharibu miili katika mji wa Al Fasher, ripoti mpya imebaini.
Utafiti wa Maabara ya Chuo Kikuu cha Yale (HRL), ambao umetumia satelaiti kufuatilia ukatili tangu vita vya RSF na jeshi kuanza, ulisema siku ya Jumanne kundi hilo "liliharibu na kuficha ushahidi wa mauaji ya halaiki" katika makao makuu ya jimbo la Darfur Kaskazini.
Kwa RSF kudhibiti eneo hilo kufuatia mapigano na jeshi katika eneo la Darfur mwezi Oktoba kulisababisha hasira kimataifa kuhusu taarifa za kuwaua watu kiholela, kubaka na kukamata watu wengi.
HRL inasema kilichofuata baada ya kuchukuwa udhibiti, imegundua makundi 150 ya viungo vinavyofanana na vya binadamu.
Vita vibaya
Mashirika ya misaada na Umoja wa Mataifa yamekuwa yakitaka kuwepo kwa njia salama kufikia Al Fasher, ambapo hakuna mawasiliano na maelfu ya walionusurika wamekwama huko, wengi wakiwa wamezuiwa na RSF.
Hakuna thibitisho rasmi la idadi ya waliouawa katika vita vya Sudan vilivyoanza Aprili 2023, huku ikikadiriwa kuwa watu zaidi ya 40,000 wameuawa.
Mkuu wa Baraza la Mpito la Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, anaongoza jeshi huku RSF ikiongozwa na naibu wake wa zamani, Mohamed Hamdan Dagalo.
Mapigano hayo pia yamesababisha mamilioni ya watu kuondoka katika makazi yao, pamoja na kuwepo kwa baa kubwa zaidi la njaa duniani.





















