Tangu Aprili 2024, mji wa El-Fasher, mji mkuu wa Jimbo la Darfur Kaskazini, umekabiliwa na mashambulizi kutoka kwa wapiganaji wa RSF. Kwa zaidi ya siku 500, raia karibu 300,000 wameshindwa kuondoka, huku watu zaidi ya 780,000 wakilazimishwa kuondoka katika makazi yao.
Upatikanaji wa chakula, maji na huduma za matibabu umekosekana. Utapiamlo miongoni mwa watoto umeongezeka kwa viwango vya kutisha, na familia zimelazimika kula ‘‘Elumbaz”— ambayo hutumika kwa lishe ya mifugo.
El-Fasher ndiyo ngome ya mwisho ya serikali ya Darfur Kaskazini, na mashambulizi ya wapiganaji wa RSF yametatiza kambi ya wakimbizi ya Abu Shouk, yakilenga maeneo ya soko, miuondombinu na ya raia kwa mashambulizi ya ndege zisizokuwa na rubani.
Wameshindwa kutoka nje ya kambi
Kulingana na ripoti rasmi ya Umoja wa Mataifa, raia 300,000 wasio na silaha wamekuwa bila huduma muhimu kwa zaidi ya mwaka mmoja, ikiwemo watoto 130,000 katika kambi za Abu Shouk na Zamzam.
Shirika la Mpango wa Chakula la WFP limeshindwa kufikisha misaada tangu mwanzoni mwa mwaka 2024, na kufikia Machi 2025, asilimia 38 ya watoto walio chini ya umri ya miaka mitano wamekuwa na utapiamlo.
Matokeo yake ni mabaya. Kati ya Aprili 2023 na Julai 2025, karibu watu 782,000 wamekimbia El-Fasher, na eneo la Tawila limepokea thuluthi nne ya watoto hao. Huku raia zaidi ya 180,000 wakiwa wameshindwa kutoka nje ya kambi ya Zamzam, wakikabiliwa na tishio la kushambuliwa vibaya wanapotaka kuondoka.
Idadi ya watu wanaopitia matatizo imeongezeka. Hospitali thelathini na tano na shule sita zimeharibiwa na haziwezi kutumika tena. Maeneo ya kuhifadhi damu, maabara, na kliniki hayafanyi tena kazi kutokana na mashambulizi ya RSF na uhaba wa bidhaa muhimu.
Upendeleo kwa waandishi wa habari
Jamii ya Kimataifa haiwezi kuruhusu El-Fasher kuwa Gaza nyingine. Huku jamii ya kimataifa ikiwa haiangazii sana masuala haya, na vyombo vya habari vikiwa haviangazii kabisa.
Kumaliza mashambulizi ya RSF inawezekana tu iwapo wanaowaunga mkono kutoka nje, hasa UAE, watajiondoa katika kutoa misaada. Bila msaada huo, uwezo wa RSF utamalizika. La sivyo, kama walivyofanya Israel huko Gaza, watoto watauawa kikatili na raia wataendelea kuuawa.
Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika lazima waongeze shinikizo kwa RSF, huku juhudi za kidiplomasia na misaada ya kifedha ikiendelezwa kwa serikali halali ya Sudan.
Ukiukwaji wa haki za binadamu uliotekelezwa na wapiganaji wa RSF lazima uchunguzwe, na waliohusika kuwajibishwa. Kwingineko, mataifa yenye uwezo katika kanda kama vile Uturuki na Misri lazima wajihusishe katika upatanishi ili kuweka msingi wa mchakato wa amani wa kudumu na unaohusisha pande zote.
Cha msingi zaidi, njia za kupitisha misaada lazima zianzishwe- kwa uratibu kati ya mashirika ya kimataifa na wadau katika kanda —kufikisha misaada kwa watu wa El-Fasher.
Mbadala wake ni hatari zaidi: njaa inayoendelea, mauaji ya kikatili, na kuangamiza idadi nyingine ya watu huku dunia isiyochukuwa hatua ikiangalia.
Mwandishi, Dkt. Mayada Kamal Eldeen Ni Profesa wa Sayansi ya Siasa na Ushirikiano wa Kimataifa, Chuo Kikuu cha Tokat Gaziosmanpaşa
Kanusho: Maoni ya mwandishi hayaakisi maoni, mitizamo na sera za uhariri za TRT Afrika.