Rais Erdogan alitoa hotuba pana katika Jukwaa la TRT World 2025 siku ya Ijumaa, akilaani mauaji ya halaiki yanayofanywa na Israel huko Gaza na kukosoa kushindwa kwa jumuiya ya kimataifa kusimamia haki, amani, na maadili.
Erdogan amehoji misimamo inayotetea Israel, akisema: "Israel ina silaha za nyuklia na uwezo wa kushambulia Gaza, popote na wakati wowote inavyotaka; inawezaji kuwa haina hatia?"
Erdogan alikosoa Israel kwa kutumia njaa kama silaha, hasa kuwalenga watoto wakati wa mojawapo ya majanga mabaya zaidi ya kibinadamu kuwahi kutokea.
"Israel inatumia njaa kama silaha mbaya, hasa dhidi ya watoto," alisema.
"Huko Gaza, hakuna hata jengo moja lililobakia. Shule, makanisa, misikiti, na hospitali zote zimeharibiwa kwa mabomu. Wanasema, 'Israel haina hatia.' Kivipi haina hatia?"
Erdogan pia alikosoa “mfumo wa propaganda ya Israel uliyojengwa kwa misingi ya uongo”, akifichua madhara yake kwa waandishi wa habari.
"Wakiwa dhidi ya mashine ya propaganda ya Israel, waandishi 270 wa habari waliotaka kufichua ukweli wa eneo hilo na kuonyesha uongo wa Tel Aviv wameuawa," alisema, akisisitiza jukumu la kimaadili la vyombo vya habari kusimama na haki.
Kiongozi wa Uturuki alikosoa taasisi za kimataifa zinazohusika na kudumisha amani na utulivu, zimefumbia macho na kushindwa kuzuia mauaji na halaiki.
"Wale waliowajibika kulinda amani ya dunia wamekosa kuzuia mauaji ya halaiki, na kuokoa maisha ya watoto," Erdogan alisema.
Mkataba wa kusitisha mapigano Gaza
Akizungumza kuhusu makubaliano dhaifu ya kusitisha vita huko Gaza, Erdogan amesema Hamas imeonyesha nia thabiti katika kutimiza masharti, huku akiikosoa Israel kwa kutafuta visingizio vya kuvunja makubaliano na kuanza mashambulio tena.
"Kila mtu anajua rekodi mbaya ya Israel linapokuja suala la kutimiza ahadi zake," alisema.
Rais Erdogan pia alionyesha matumaini kuhusu mgogoro wa Urusi na Ukraine, akisema Uturuki inaamini "suluhu la kati litapatikana hivi karibuni" ili kuruhusu mataifa yote kushirikiana na kuishi pamoja kwa amani.
Akithibitisha sera za kigeni zenye misingi thabiti za Uturuki, Erdogan alisema Ankara “inakemea vikali ukatili unaofanywa dhidi ya raia” huko Al Fasher, Sudan, na kuhimiza hatua za haraka kuzuia ghasia.
Jukwaa la kila mwaka la TRT World huwaleta pamoja watunga sera, wanasayansi, na wahariri wa habari kutoka duniani kote kujadili changamoto muhimu za kimataifa, huku mjadala wa mwaka huu ukizingatia maadili, haki, na mageuzi katika mpangilio wa dunia.
Ukifanyika chini ua kaulimbiu "Marekebisho ya Dunia: Kutoka Utaratibu wa Zamani hadi Uhalisia Mpya", tukio la siku mbili litaangazia jinsi mabadiliko katika uchumi, teknolojia, vyombo vya habari na sheria za kimataifa zinavyobadilisha dunia tunayoishi.


















