Bei za petroli na rejareja zimeendelea kushuka nchini Tanzania kwa mwezi Oktoba 2024, ukilinganisha na mwezi Septemba.
Kwa mujibu wa taarifa iliyowekwa kwenye ukurasa wa X wa EWURA siku ya Oktoba 2, 2024, watumiaji wa nishati ya petroli jijini Dar es Salaam, sasa watalazimika kulipia Dola za Kimarekani 1.10 (Shilingi za Kitanzania 3,011) kwa lita moja ya nishati hiyo kwa bei ya rejareja, ukilinganisha na Dola 1.20 (Shilingi za Kitanzania) 3,231)kwa mwezi Septemba.
Taarifa hiyo ya EWURA inasema kuwa bidhaa ya dizeli nayo imeshuka kutoka Dola 1.10 (Shilingi za Kitanzania 3,011) kwa mwezi Septemba hadi Dola 1.04 (Shilingi za Kitanzania 2,846) kwa mwezi Oktoba, 2024.
Mamlaka hiyo imesisitiza kuwa bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko, kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015, kifungu namba 166.
“Bidhaa za mafuta zinazoagizwa na kupokelewa nchini zinazingatia bei za mafuta yaliyosafishwa kutoka soko la Uarabuni. Oktoba 2024, bei za kikomo za mafuta zimekokotolewa kwa kuzingatia bei za soko la Uarabuni za Septemba 2024,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Pia, imevitaka vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana yakionesha bei za mafuta, punguzo, vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika.