Soko la Machinga Dodoma. Picha/TRT Afrika.

Ronald Sonyo

TRT Afrika, Dodoma, Tanzania

Soko jipya la kisasa maarufu ‘Machinga Complex’ lililopo Dodoma, Tanzania linaonekana kuanza kuwa mkombozi kwa maelfu ya wachuuzi ambao awali hawakuwa na maeneo maalum ya kufanya biashara.

Kwa mujibu wa Serikali ya Tanzania, mradi huo uliogharimu kiasi cha fedha za Kitanzania bilioni 9.5 ulilenga kupunguza msongamano wa mji na uchafu unaozalishwa kutokana na shughuli za uchuuzi.

Ingawa hatua ya kuwahamisha maelfu ya wachuuzi waliokuwa mitaani mjini humo, awali ilipata upinzani na kulalamikiwa kwa madai kwamba, sehemu iliyotengwa haikuwa nzuri kibiashara lakini pia ilikosa miundombinu muhimu ikiwemo kituo rasmi cha magari ya usafiri wa umma maarufu daladala zinazotoka na kuingia mjini. Wengi waliiona hatua hiyo kwamba ingedhoofisha biashara.

Hata hivyo, kama sehemu ya utekelezaji wa agizo lililotolewa na rais wa nchi hiyo Samia Suluhu Hassan, la kuwahamisha wachuuzi hao lakini kwa njia ya staha, uongozi wa jiji la Dodoma ulitetea msimamo wake na kusema kwamba hatua hiyo ilikuwa ni muhimu na ililenga kuboresha mazingira rafiki ya biashara pamoja na upanuzi wa mji.

Wachuuzi wa nguo za mitumba wakiwa wamepanga bidhaa zao katika moja ya barabara maarufu Nyerere Square jijini Dodoma. Picha/TRT Afrika.

Hali ilivyo sasa

Ni takriban mwaka mmoja sasa tangu soko hilo lilipoanza kutumika na kubadili kabisa taswira ya mji. Ingawa awali kulikuwa na changamoto kadhaa, lakini kadri siku zinavyokwenda, uongozi wa jiji umekuwa ukiendelea na jitihada za kuboresha mazingira ya soko hilo, ikiwemo uanzishaji wa kituo cha magari ya usafiri wa umma pamoja na kuweka vyumba maalumu kwa ajili ya kina mama kuweza kunyonyesha na kulaza watoto wao pindi wanapokuwa kazini.

Licha ya awali kuonekana kuna kusuasua kwa wachuuzi kuhama katika soko la Machinga Complex, hivi sasa soko hilo lina takriban wachuuzi 3500 walihamishwa, wengi wao ni wale waliokuwa wakifanya biashara barabarani ikiwemo barabara maarufu kama Nyerere Square na One Way.

Muonekano wa barabara maarufu One Way ambayo ilikuwa inatumiwa na machinga kuuza bidhaa mbalimbali. Picha TRT Afrika.

Wachuuzi wanasemaje?

Wengi wanafurahi kwa kupata nafasi ya kujiamulia wakati gani wafungue na kufunga biashara, lakini Devota Atanasi pengine ana furaha zaidi. Awali alikuwa akipanga bidhaa zake pembezoni mwa barabara, ambapo aliruhusiwa tu kufanya hivyo, kuanzia saa kumi jioni. Lakini hivi sasa, baada ya kuhamia Machinga Complex, ameweza kuongeza muda wa kufanya biashara kuanzia asubuhi mpaka jioni.

“Nilikuwa Square kwenye jua kali, lakini sasa nipo kivulini na ninajiamulia muda wa kufunga, siwezi tena kurudi Square hata kama kuna wakati nakosa wateja lakini ni kawaida, nafurahi sana,” alisema.

Baadhi ya wafanyabiashara wadogo wakiwa katika Soko la Machinga jijini Dodoma, Tanzania. Picha/TRT Afrika.

Sio wote wenye ndoto ya kusalia hapa

Sharifa Maulid ni muuza mboga. Awali alikuwa katika Soko Kuu la majengo, yeye hamu yake ni kurudi Soko la Majengo kwa sababu anasema, kulikuwa na biashara tofauti na alipo sasa.

”Natamani kweli kurudi Majengo kwa sababu kule kulikuwa na daladala na biashara ila hizi daladala zilizopo zinashusha na kuondoka sasa ndio nini?" alihoji na kisha akaendela, "Tuletewe daladala za Nkuhungu na Mnadani maana hiyo ndio kila kitu,” alisema.

"Mwanzo nilikuwa nafanya biashara katikati ya mji 'One Way' nilikuwa na hofu na sikujua hatma yangu huku nikikabiliwa na changamoto za kimazingira," alisema Prosper Malya mfanyabiashara wa soko hilo.

Ingawa alipongeza hatua ya Serikali ya kuwajengea soko, lakini alitamani Serikali kukomesha vituo bubu vya daladala ambavyo Machinga hawanufaiki navyo.

"Mwanzo nilikuwa nafanya biashara katikati ya mji 'One Way' nilikuwa na hofu na sikujua hatma yangu."

Prosper Malya, mfanyabiashara wa Soko la Machinga Complex, Dodoma.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri ameelezea kufurahishwa kwake baada ya kuona kuona machinga wamewekwa katika eneo rasmi kwa ajili ya kazi zao. Ingawa hakutoa idadi kamili lakini alikiri kuongezeka kwa kundi hilo, hivyo kuifanya serikali kubuni masoko mengine yatakayokidhi mahitaji ya wachuuzi bila kuwaathiri kiuchumi.

"Nina furaha sana kwamba tumefuata maelekezo ya Rais yaliohitaji kiwango kikubwa cha tahadhari wakati wa kuhamisha machinga na tumetafsiri maono yake. Na sisi hatukuamini kama zoezi lingefanikiwa bila kutumia nguvu, lakini sasa nina amani,” amesema Mkuu huyo wa Wilaya.

Pia aliongeza kusema kuwa bado kuna maboresho zaidi yanayoendelea kufanyika ikiwemo kuimarisha barabara za kiwango kwa kiwango cha lami na taa za barabara pembezoni mwa soko.

Sehemu ya soko la Machinga Dodoma ambayo inahitaji maboresho ya miundombinu ya barabara. Hali hii imekuwa ikilalamikiwa na baadhi ya wamiliki wa magari pamoja na wafanyabiashara sokoni hapo. Picha: TRT Afrika

‘’Mafanikio makubwa ni kurasimisha ile biashara, kuaminika kwa wachuuzi na kutengeneza fursa ya kufikiwa na taasisi mbalimbali za kifedha, siku za nyuma usingeweza kumkopesha machinga usiyejua ni wapi anakaa na ilikuwa pia vigumu kuwafikia kwa wakati mmoja” Alisema na kuongeza wakina mama wenye watoto hawakuwa na chumba cha kunyonyesha lakini sasa kipo na huduma za Afya ” Alisema.

Ingawa wachuuzi wamepokea hatua hii kwa furaha lakini wanataka uboreshaji zaidi ufanyike. Sehemu kubwa ya wachuuzi hawa ni vijana waliohitimu katika vyuo mbalimbali vya elimu ya juu na kujiingiza katika shughuli kama hizi kama sehemu ya ajira bila kujali fani walizosomea.

Jabir Shekimweri, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma. Picha/TRT Afrika

Nchini Tanzania, kumekuwa na utelekelezaji wa ajigo la Rais wa nchi hiyo la kuondolewa kwa machinga katika miji mikubwa kama sehemu ya kusafisha mji lakini pia kuwatengea maeneo maalumu. Hata hivyo Samia Samia amekuwa akitilia mkazo kwamba hamisha hiyo ifanyike kwa weledi na staha.

Hata hivyo, jambo ambalo linaweza kutia doa jitihada hizo za kuwaweka sehemu moja wachuuzi, ni kuanza kuonekana kwa baadhi ya wachuuzi kurudi katika maeneo ambayo yamepigwa marufuku. Baadhi ya wataalamu wa mipango miji, wanasema ni muhimu kwa serikali kuwa macho na kuhakikisha wale wote walioondolewa hawarudi tena mjini.

TRT Afrika