Mgodi wa Kilembe iko katika wilaya ya Kasese katika eneo la Magharibi mwa Uganda. / Picha: Reuters

Waziri wa Nchi anayeshughulikia uwekezaji nchini Uganda, Evelyn Anite, alitangaza kwamba Uganda imesimamisha mkataba wake na Tibet-Hima, mfanyabiashara wa Mgodi wa Kilembe wa kutoka Uchina.

Mgodi wa Kilembe uko katika Wilaya ya Kasese katika eneo la magharibi mwa Uganda.

Waziri Anite alisema hii baada ya mwekezaji huyo kutaka kusafirisha tani 30,000 za dhahabu, shaba na kobalti kama sampuli kwa ajili ya majaribio nchini China.

Anite aliyasema hayo alipofika mbele ya Kamati ya Bunge ya Maliasili, ambapo aliitwa kueleza hatua iliyofikiwa ya ufufuaji wa Migodi ya Kilembe Wilayani Kasese.

“Mkandarasi huyu alitaka serikali imruhusu kuchukua tani 30,000 za shaba, kobalti na dhahabu kwa ajili ya sampuli tu. Haikuwa busara kwa mwanakandarasi kufikiria kwamba tungeruhusu kiasi kikubwa kama hicho cha maliasili kuondoka nchini,” Anite alieleza.

Alieleza sababu kuu za kusitishwa kwa mkataba huo .

Kwanza wingi wa bidhaa ambazo mwekezaji alitafuta kwa ajili ya majaribio, pili madai kuwa mgodi ulijaa maji, na tatu baadaye ugunduzi wa uzembe wa mwekezaji kusimamia operesheni hiyo kubwa.

“Rais ( Yoweri Museveni) alisema kuwa rasilimali hizi ni za Wananchi wa Uganda. Tibet-Hima walipogundua hilo, walionyesha kwamba hawataendeleza mkataba huo, kama ilivyobainishwa katika ripoti ya tume. Ilikuwa ni jambo lisilokubalika kwa Rais, kwangu na kwa Serikali kwa ujumla,” alisema Anite.

Mamalamiko ya kampuni ya Tibet-Hima

Uchunguzi wa Bunge kuhusu kandarasi hiyo ya uchimbaji wa madini ulianzishwa kufuatia ombi la Solomon Silwany mbunge wa Bukooli ya Kati, Aprili 2024, lililoomba uchunguzi kuhusu mazingira ya kusitishwa kwa mkataba wa kampuni ya Tibet-Hima wa kusimamia, kukarabati na kuendesha Migodi ya Kilembe kwa miaka 25.

Kwa mujibu wa Silwany, Serikali ilishindwa kutimiza wajibu wake chini ya mkataba huo, hivyo kusababisha kampuni ya madini ya Tibet-Hima kupata hasara ya dola milioni 980 (shilingi trilioni 3.581) kati ya 2014 na 2017.

“Kampuni ilitoa shilingi bilioni 4.2 kwa serikali, ikaajiri wananchi 822 moja kwa moja, akanunua vifaa vya thamani ya dola milioni 22 (shilingi bilioni 80.411 ), na alitoa dola milioni 183.5 (shilingi bilioni 676.187) kwa uwekezaji wa siku zijazo katika kurejesha uzalishaji wa madini ya shaba kutoka kwa Kilembe, ” Silwany aliiambia Kamati ya Bunge.

Kampuni ya Tibet-Hima Ltd pia ilitaja malalamiko kadhaa dhidi ya Serikali ya Uganda, kuwa ni pamoja na kushindwa kukabidhi eneo la Mgodi wa Kilembe ndani ya miezi tisa baada ya kusainiwa kwa mkataba na uamuzi wa Serikali kupunguza muda wa mkataba kutoka miaka 25 hadi 15 na hivyo kusababisha kusitishwa kwa mkataba.

Waziri Anite alielezea kamati ya Bunge kuwa hajutii uamuzi wake wa kusitisha mkataba na Tibet-Hima.

TRT Afrika