Kiwanda hicho kilojengwa kwa gharama ya dola milioni 20 kitatengeneza dawa zitakazosaidia kuokoa hasa maisha ya kina mama wanaotokwa na damu nyingi baada ya kujifungua. Pia kitatengeneza dawa za kupunguza maumivu.
Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya Piston Medical Limited Bw. Benjamin Kiiza alisema wakati wa uzinduzi kuwa shirika lake lilianza kuagiza dawa kutoka nje na kuuza nchini kabla ya kuamua kujenga kiwanda chao wenyewe.
''2019 tulianza kutengeneza baadhi ya dawa ambazo tulikuwa tunaagiza kutoka nje'', aliongeza Kiiza
Katibu Mkuu wa Wizara ya afya Uganda Dkt. Diana Atwiine ameahidi kuwa serikali itaendelea kununua dawa za kampuni ya Piston cha msingi tu wazingatie ubora na bei iwe nafuu.
Wakati wa uzinduzi huo rais Museveni alisema serikali itaangalia kwa makini suala la kupunguza gharama za umeme na kutengeneza barabara nzuri. Alieleza kufurahishwa kwake kwa kile alichokitaja kuwa ''anafarijika kumuona mtu akitoka kijijini na kuwa muwekezaji mkubwa''
Dawa nyingi zitakazotengenezwa zitatumia mfumo wa kuchoma sindano
Kulingana na ripoti ya utafiti wa masuala ya afya 2022 wanawake 189 kati ya wajawazito 100,000 walifariki dunia nchini Uganda. Vifo hivyo vilitokea wakati wa ujauzito, kujifungua au siku 40 baada ya kujifungua.















