Mwanaharakati Elizabeth Herriman kutoka Marekani akiwa katika mtando wa kijamii wa Tiktok / Picha: Wengine

Na Elizabeth Herriman

Kukua kwangu baada ya matokeo ya Septemba 11 Marekani, kama asiyekuwa Muislamu, mimi si mgeni na Islamophobia - chuki dhidi ya Uislamu.

Kuanzia kumtazama Jeff Dunham akiwa na kibaraka wake, Achmed the Dead Terrorist kwenye Comedy Central, hadi kuona watu karibu nami wakiamini uvumi ya kuwa Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama alikuwa Mwislamu kwa siri, na kusikia wavulana wa darasa langu wakipiga kelele, "Allahu Akbar", huku wakifanyia mzaha kuhusu walipuaji wa kujitoa mhanga - kuwafanyia mzaha na kuwaharibia Waislamu jina, ni jambo ambalo limefanywa kuwa la kawaida kila mahali nchini Marekani.

Wengi nchini Marekani wanahusisha Uislamu na wafuasi wake na migogoro katika Mashariki ya Kati, ingawaje ni dini tofauti sana na wafuasi kutoka duniani kote.

Uhusishaji huu umewekewa makusudi na unasukumwa na baadhi ya wanasiasa ili kurahisisha kuhalalisha vita na ghasia katika nchi nyingine. Madhara yanayotarajiwa yanazidi kuwa wazi, kwani tumeshuhudia chuki dhidi ya Uislamu ikiendelea katika mauaji ya halaiki ya Wapalestina huko Gaza.

Waandamanaji wanaoungo mkono Palestina wakiwa New York / Picha: Leonardo Munoz

Tangu matukio ya Oktoba 7, mimi, kama Wamarekani wengine wengi, nilianza kuzama ndani na kujifunza zaidi kuhusu migogoro inayotokea Mashariki ya Kati, nikiichunguza kwa mara ya kwanza.

Nilichogundua ni kwamba sipendi jinsi serikali yangu inavyotumia pesa zangu za ushuru kufadhili mauaji ya raia wasio na hatia. Hakuna mshangao hapo. Kama tu Waamerika wenzangu wengi, nilianza kugomea makampuni kwenye orodha ya kususia vuguvugu la Boycott, Divestment, Sanctions (BDS) ili kujaribu kuzuia pesa zangu kwenda kwa mifuko ya watu wanaolenga kuzitumia kwa vurugu.

Nilichojifunza wakati huo ni kwamba, katika nchi yenye utamaduni mzima unaojengwa kwenye matumizi ya bidhaa, ni vigumu sana kuacha matumizi. Wakati huo huo nilipokuwa na mapambano haya ya ndani kati ya maadili yangu na uraibu wangu, nilianza kuona machapisho kwenye TikTok ya Waislamu wakijiandaa kwa Ramadhan.

Nilipotafuta habari kuhusu Ramadhan, nilipata maadili ya msingi ya mwezi mtukufu inajumuisha kile nilichokuwa nikijaribu kuomba ndani mwangu. Kwa hiyo niliamua kufunga mwezi wa Ramadhani nikiwa si Muislamu ili kuona ni nini ninachoweza kujifunza kutokana nayo.

Nilipotengeneza video yangu ya kwanza ya TikTok kuhusu Ramadhan na kuituma kwenye akaunti yangu, nilikuwa na wafuasi 300. Akaunti yangu imeongezeka na kufikia zaidi ya wafuasi 20,000 tangu kuchapisha video hiyo, na ninatumai kuwa ninaweza kuwafikia watu wengi zaidi ambao wamekuwa wakipitia mapambano kama yangu. Ninawatia moyo wajifunze zaidi kuhusu dini ambayo mara nyingi inaharibiwa katika vyombo vyetu vya habari.

Video ya kwanza ilifikia wengi kwa Waislamu na wasio Waislamu. Sikuwa na mpango wa kufanya mfululizo wa video hizi, lakini baadhi ya watoa maoni walipotoa pendekezo hilo, niliona fursa ya kupambana na suala ambalo nilikuwa naliona, wakati wa kutetea ukombozi wa Palestina.

Mara kwa mara, watu ninaowafahamu wamekuwa wakiwalinganisha Waislamu na Uislamu na Hamas na baadaye, ugaidi. Simulizi hii kwamba ikiwa wewe ni Mwislamu na/au kutoka Mashariki ya Kati, basi wewe ni gaidi, si geni.

Propaganda zinazoenezwa kuhusu Uislamu na kile ambacho wafuasi wake wanadaiwa kuunga mkono zimezuka tena vibaya katika kipindi cha miezi sita iliyopita huku Gaza ikishambuliwa kikatili. Mara kwa mara naona watu wanatumia Islamophobia kuhalalisha propaganda hizo.

Miongoni mwa maoni yote mazuri na ya kutia moyo kwenye video yangu, pia kulikuwa na matamshi ya kashfa ya kawaida unayoona dhidi ya Waislamu. Kwa hiyo niliamua kwamba nikiwa nafunga Ramadhan, nilitaka kushiriki jaribio langu na kutengeneza video zinazopinga imani potofu kuhusu dini.

Hadi sasa nimetoa sadaka, kusoma baadhi ya Quran, kuvaa hijabu, kushiriki habari kuhusu ukweli wa Uislamu na watu wote wazuri wanaoufuata, na nimekaribishwa kwa maneno ya uchangamfu sana.

Msanii Elizabeth Herriman aeleza aliyojifunza akiwa amefunga swaumu ya Ramadhan ilhali akiwa si Muislamu. Picha: Wengine

Nimepata jumuiya ya watu wanyenyekevu na waaminifu ambao sijawahi kukutana nao. Upendo ambao nimeonyeshwa na jumuiya ya Kiislamu umeshinda kwa kiasi kikubwa upinzani wowote ambao nimepata. Mpenzi wangu na familia yake wamekuwa wakiniunga mkono sana, jambo ambalo limekuwa baraka.

Pia nimeweza kutumia jukwaa langu jipya kuzungumzia Palestina na kusaidia kushiriki uchangishaji fedha ili kuhamisha familia kutoka Gaza na kusisitiza jinsi ilivyo muhimu kuwa na usitishaji vita wa mara moja na wa kudumu.

Kufunga swaumu imekuwa ngumu lakini yenye faida. Kila mtu alikuwa akiniambia kwamba siku tatu za kwanza zingekuwa ngumu zaidi, na walikuwa sahihi. Siku hizo chache za kwanza, niliweza kuhisi uchungu wa njaa sana wakati wa mchana, na sikuwa na uhakika kama ningeweza kufanya hivyo kwa mwezi mzima.

Tende ni tuna linalopendwa kuliwa siku za Ramadhan / Picha: Getty

Lakini mwisho wa siku, ninapoweza hatimaye kufuturu, ninahisi hisia tofauti ya shukrani ninapo kula chakula na kunwya maji kuliko kawaida. Ninahisi nimefanikiwa kufanya jambo na ninahisi kujiamini zaidi katika uwezo wangu wa kujiwekea nidhamu.

Kufikia sasa, ni rahisi sana kufunga wakati wa mchana na ninaweza kuzingatia zaidi kipengele cha kutoa sadaka kwa wengine katika mwezi mtukufu, kwa hivyo ninatafuta njia zaidi za kumaliza Ramadhan kujaribu kurudisha wema kawa umma wa Kiislamu kwa kadri walivyonipa.

Hivi mwezi wa Ramadhan unavyo kwenda kwisha, nimefanya mipango na wanaharakati wengine na mashirika kama vile Operation Olive Branch kutumia TikTok mubashara ili "Kuwapokea Familia" kutoka Gaza na kusaidia kurahisisha michango kwa kampeni zao za GoFundMe ili waweze kuhama eneo hilo.

Nimepata njia kadhaa mbadala za kutumia pesa mbali na kutumia shirika zinazounga mkono mauaji ya halaiki kama vile kuwekeza katika maduka ya mitumba, kununua kutoka kwa biashara ndogo ndogo (ikiwezekana zinazomilikiwa na Wapalestina) na kutumia programu kama vile No Thanks ambazo hukusaidia kuzuia shirika zinazosaidia Israeli.

Jaribio langu katika Ramadhan hii limekuwa la ajabu na nimejifunza mengi.

Nafikiri kwamba yeyote anayependa kujifunza zaidi kuhusu Uislamu anapaswa kufanya hivuo kwa sababu watapata mikono iliyokunjuliwa na mioyo mizuri ikiwangoja.

Mwandishi, Elizabeth Herriman ni mwimbaji/mtunzi wa nyimbo na mwanaharakati wa Marekani ambaye anaishi na mpenzi wake na paka watatu katika milima ya Colorado.

TRT Afrika