Kuna mchezo unaoendelea katika jukwaa la kimataifa. Mchezo wa dhahabu na mhusika mkuu ni Marekani.
Kama umekuwa ukifuatilia mauzo ya dhahabu duniani, kumekuwa na wimbi kubwa la taasisi za fedha ikiwemo benki kuu za mataifa mbalimbali kununua na kuhodhi dhahabu kwa kiwango kikubwa.
Hii sio bahati mbaya ila ni mfumo makusudi unaotumiwa kujikinga na athari za kutokea kwa mdororo wa uchumi wa dunia. Hiyo ndio hofu kubwa iliyopo.
Marekani inahusika vipi?
Kimsingi kwa sasa Marekani iko taabani kutokana na deni lake la taifa hasa madeni ya nje.
Marekani imekopa takriban dola trilioni 35. Na kwa deni hili inalipa riba ya kila mwaka ya dola trilioni moja.Lakini ndani ya nchi mambo ni magumu.
Ukusanyaji wa fedha haukidhi ulipaji deni na kuendeleza miradi ya kitaifa ikiwemo gharama za huduma za umma.
Kwa hiyo Donald Trump anatafuta ni njia ya kujikwamua, na lipi chaguo lake?Kwa sasa Marekani ndio ina akiba kubwa zaidi ya dhahabu katika mabenki yake.
Ukadiriaji upya wa hifadhi za dhahabu
Thamani ya dhahabu yake hata hivyo bado imekadiriwa kwa viwango vya tangu mwaka 1973, ikiweka thamani yake takriban dola bilioni kumi na mja.
Kwa hiyo iwapo serikali ya Marekani itaamua kufanya makadirio mapya ya thamani ya dhahabu yake, huenda ikazidi dola trilioni moja yaani itakuwa zaidi ya asili mia tisini ya thamani yake ya ujazo.
Iwapo hili litafanyika, kuna uwezekano kuwa hifadhi za Marekani za dhahabu zikamudu kulipa takriban nusu ya deni lake.
Haitakuwa mara ya kwanza kwa nchi kufanyia makadirio mapya ya thamani yake ya dhahabu, kwani ishafanyika Ujerumani, Afrika Kusini na Italia, ambapo iliwawezesha kulipa madeni yao ya nje.
Tishio kwa thamani ya sarafu ya Dola
Changamoto ya Marekani kufuata mkondo huu, ni kuwa itasukuma zaidi ukosefu wa imani kimataifa kwa sarafu ya dola ya Marekani kama mdhamini.
Hii ikimaanisha thamani ya dola kimataifa itaanguka. Hii pia itasababisha nchi zaidi kufuata mkondo kama huu, na hivyo kusukuma thamani ya dhahabu juu kupita kiasi.
Ndio ni njia mojawapo ya Marekani kujikwamua kutoka deni kubwa la nje. Lakini kumbuka kushusha thamani ya dola ina hatari kubwa ndani ya Marekani kwani inaweza kuwa sababu ya serikali kukosa umaarufu kutokana na hasira za wananchi.
Kwa hiyo hatua za Trump kuhusu dhahabu ya Marekani inasubiriwa na wengi.Lakini wakati wanasubiri, kama tulivyotaja awali, benki kuu za dunia zimeanza kununua na kuhodhi dhahabu kwa kiasi kikubwa kama sehemu ya tahadhari.