| Swahili
AFRIKA
7 DK KUSOMA
Sudan ilikuwa kimbilio salama kwa wakimbizi sasa ni chanzo cha wakimbizi
Dunia ikiadhimisha Siku ya Wakimbizi Duniani 20 Juni, Sudan imeangaziwa huku takribani watu laki tano wakiripotiwa wamekimbia makwao kutokana na vita iliyoanza Aprili 15 mwaka huu
Sudan ilikuwa kimbilio salama kwa wakimbizi sasa ni chanzo cha wakimbizi
UN wanasema watu karibia laki tano wamelazimika kuwa wakimbizi kwasababu ya vita nchini Sudan  / Picha: Reuters / Reuters

Na Coletta Wanjohi

Maisha yalikuwa ya kiwewe kwa watoto katika kituo cha watoto yatima cha Maygoma katika mji mkuu wa Sudan Khartoum, wakati mapigano yaliongezeka kati ya jeshi la Sudan na vikosi vya Msaada wa Haraka, RSF, yakizidi katika mji mkuu wa Sudan.

Nyumba hiyo ambayo ilitunza watoto 280 ilikuwa mita 800 tu kutoka maeneo ya vita.

"Mapigano yalipozuka meneja wa kituo cha kulelea watoto yatima alijaribu sana kuwashawishi wafanyakazi waliokuwa wakifanya kazi hapa kubaki," alieleza Abeer Abdullah, mlezi wa watoto hao," baadhi ya wafanyakazi walikaa kwa siku kadhaa lakini kwa kuwa walikuwa na wasiwasi kuhusu wapendwa wao ilibidi waondoke hatimaye.”

Timu kutoka kwa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, ICRC, iliwahamisha watoto hao na walezi wao 70 hadi Wad Mani takriban kilomita 200 kutoka Khartoum.

Uhamisho wa lazima umekuwa maisha ya watu kwa wengi kama watoto hawa ambao walipatikana katikati ya mzozo wa kijeshi tangu Aprili 15 ulipoanza.

Nchini Tanzania, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili jijini Dar es Salaam, kimepokea wanafunzi 150 wa udaktari kutoka Sudan ambao elimu yao imetatizika kutokana na mzozo huo.

Watamaliza mwaka wao wa mwisho wa masomo hapa.

" Wanafunzi hawa, kila mmoja wao alikimbia na wazazi wao kutokana na mapigano nchini Sudan," anaeleza Mohamed Janabi, Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, "tumewaruhusu kumaliza mwaka wao wa tano wa shule ya matibabu hapa katika hospitali yetu."

Katika mipaka ya Chad, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Misri na Ethiopia, mashirika ya misaada ya kibinadamu yanaripoti kufurika kwa wakimbizi pia.

Maelfu hawaja bahatika kuhamishwa kwa utaratibu maalumu kama watoto waliokuwa katika kituo cha watoto yatima na wanafunzi wa udakitari waliopelekwa Sudan.

"Tangu mzozo kuanza , zaidi ya watu milioni 2.1 wamekimbia mapigano. Takriban nusu milioni wamevuka na kuingia katika nchi jirani, nyingi zikiwa tayari zinakabiliwa na majanga yao ya kibinadamu." Martin Griffiths, Naibu Katibu Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu na Mratibu wa Misaada ya Dharura aliambia mkutano wa kuahidi Jumatatu.

Hali imebadilika

Kabla ya mzozo wa mwezi Aprili, Sudan ilizingatiwa kuwa mwenyeji wa mojawapo ya idadi kubwa ya wakimbizi barani Afrika inayowapa hifadhi wakimbizi milioni 1.1.

Takriban 800,000 walitoka nchi jirani ya Sudan Kusini ambako vita vya ndani tangu mwaka 2013 umewakosesha makazi raia wengi.

Wakimbizi wengine wanatoka Eritrea na Ethiopia.

Lakini sasa Sudan imekuwa chanzo kikubwa cha wakimbizi.

"Tumerekodi wakimbizi 365,000 tangu kuanza kwa mzozo huu, huku Misri na Chad wakiwa wenyeji wengi, lakini watu pia wanakimbilia nchi jirani," Philipo Grande, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Wakimbizi alisema Jumatatu.

"Inawezekana tumebakisha siku chache tu kabla ya msimu wa mvua ambao utazidisha mateso ya mamia ya maelfu waliokimbia, na kupunguza zaidi uwezo wetu kufika katika maeneo ya vijijini na ya mbali, kwa mfano, mashariki mwa Chad na Jamhuri ya Afrika ya Kati.” aliongeza.

"Nilijionea hali mbaya ya Wasudan wengi wanaofika Misri - wakiwa wamepungukiwa na maji, wamechoka, wengi wakihitaji msaada wa matibabu."

Hali ni ngumu zaidi kwa baadhi ya Wakimbizi kutoka Sudan Kusini waliokimbia vita katika nchi yao wakati mzozo wa ndani ulipoanza mwaka 2013 na sasa wanalazimika kurejea katika hali ile ile waliyoikimbia.

"Wakimbizi wa Sudan kusini wapatao 113,000 hadi sasa wamelazimika kurudi katika nchi yao ya asili bila chochote. Wanarudi katika maeneo ambayo hayako tayari kuwapokea kwa sababu ya kutokuwa na usalama ,” Grande aliongeza.

Shirika la Kimataifa la Misaada ya Kibinadamu, Medecins Sans Frontieres, MSF, linaonya kuhusu ripoti za watu kupigwa risasi na kuuawa walipokuwa wakijaribu kuondoka Darfur Magharibi.

Inasema Wasudan 15,000, kati yao 900 waliojeruhiwa wamewasili Chad kwa muda wa siku nne zilizopita kutoka Sudan.

"Jumatano usiku tarehe 14 Juni, gavana wa Darfur Magharibi aliuawa. Kwa wakati huu tulijua kwamba hali ingezidi kuwa mbaya zaidi, na ulikuwa uamuzi wa pamoja wa watu wa El Geneina kuondoka,” aeleza Nour mwenye umri wa miaka 25, aliyefika katika hospitali ya Adre, nchini Chad.

El Genaina ni mji mkuu wa jimbo la Darfur Magharibi, moja ya maeneo ambayo mapigano ni makali.

“Niliona watu wengi waliokufa na waliojeruhiwa wakiwa wamelala chini. suluhisho pekee kwetu lilikuwa kuelekea Magharibi na watu wakaanza kutembea hadi Adre, nchini Chad,” Nour aliongeza.

Mahitaji yanaongezeka

Kulingana na Umoja wa Mataifa watu milioni 24.7, karibu nusu ya wakazi wa Sudan sasa wanahitaji misaada ya kibinadamu na ulinzi.

Hii inajumuisha walio ndani ya nchi na wakimbizi katika nchi jirani. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi linasema Mpango wa Kukabiliana na Wakimbizi wa Kikanda wa Sudan unatafuta dola milioni 566.4 kusaidia wakimbizi, waliorejea na jumuiya zinazowahifadhi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Misri, Ethiopia na Sudan Kusini.

Fedha hizo zinalenga msaada kwa zaidi ya watu milioni 1.2, wakiwemo wakimbizi, waliorejea na raia wa nchi zingine.

Kufikia sasa mahitaji haya yamepokea ufadhili wa asili mia tu ya fedha zizlizohitajika.

"Ninatenga leo nyongeza ya dola milioni 22 kutoka Mfuko Mkuu wa Makabiliano ya Dharura kushughulikia mahitaji ya kipaumbele," Griffith alisema Jumatatu "dola milioni 25 tayari zimetengwa, kutoka kwa hazina hii, kusaidia juhudi za kibinadamu katika nchi jirani."

Hazina hii ya dharura imechangia dola milioni 65 kukabiliana na mzozo mwaka huu.

Kongamano la maslahi ya Sudan uliowakutanisha nchi tofauti ulitangaza ahadi ya karibu dola bilioni 1.5 kwa ajili ya kufadhili juhudi za kuokoa maisha nchini Sudan na kandani.

Umoja wa Afrika unatetea mchakato wa amani unaoongozwa na Afrika ili kukomesha mapigano nchini Sudan.

Mamlaka ya Kiserikali ya Maendeleo, IGAD ambayo Sudan ni mwanachama, imeteua kamati ya nchi 5 kuanzisha mchakato wa amani kwa Sudan.

Kwa Wananchi wa Sudan wengi waliolazimika kuondoka nyumbani, kutokuwa na uhakika kumekuwa kitu kawaida cha kila siku.

Wanachotaka ni kurudi nyumbani.

CHANZO:TRT Afrika