Dayo Yussuf
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Kufikia Disemba 2023, jumla ya nchi 12 za Afrika zilifanya uchaguzi wao. Onyesho la demokrasia katika bara ambalo kwa miaka mingi lilionekana kuwa, hebu tuseme sio kidemokrasia sana.
Lakini Waafrika wameazimia kuuthibitishia ulimwengu wote kuwa taswira ni tofauti. Katika miongo michache iliyopita, nchi nyingi zimehama kutoka katika utawala wa chama kimoja, udikteta, na uongozi kwa mkono wa chuma, na kwenda kwenye mabadiliko ya amani ya madaraka, kwa lengo kuu, kufikia amani. Bila amani hakuna maendeleo.
Hata hivyo, uthabiti wao na nia yao imejaribiwa kwa mwaka mzima, na bado bara hili linasimama imara likiwa na shauku kubwa zaidi ya mabadiliko kwa manufaa ya watu wake.
Migogoro kwa takwimu
Cha kusikitisha ni kwamba, bara hilo bado linashikilia rekodi ya kuwa na idadi kubwa zaidi ya migogoro. Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi UNHCR na lile la Uhamiaji la IOM wanasema angalau watu milioni 40 katika bara hilo wamekimbia makazi yao mwaka huu pekee kutokana na masuala mbalimbali, lakini zaidi migogoro.
Na hapa tunazungumzia wakimbizi wa ndani au waliokimbia na wanaotafuta hifadhi nje ya nchi zao au hata nje ya bara.
Lakini kati ya zaidi ya watu milioni 40 waliokimbia makazi yao, 77% wanaaminika kuwa wakimbizi wa ndani. Hii inatia doa juhudi zilizotajwa mwanzoni, kujitahidi kuleta amani barani Afrika.
Takwimu za hivi punde zaidi zilizotolewa na IOM na UNHCR zinaonyesha angalau nchi 15 za Kiafrika zimezama katika migogoro ya ndani ambayo imesukuma idadi kubwa ya watu wao kukimbia.
Wahusika wakubwa ni Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambazo, kwa pamoja, zina karibu watu milioni 15 wanaotafuta hifadhi katika nchi jirani.
Sudan
Ingawa kulikuwa na mapigano na mashambulizi yaliyoenea sehemu nyingi za Afrika tangu mwanzoni mwa mwaka, Aprili 15 ilikuja kama mshtuko mkubwa sio tu kwa Bara lakini kwa ulimwengu wote.
Mapigano makali yalizuka kati ya Wanajeshi wa Sudan (SAF) na Wanajeshi wa Msaada wa Haraka (RSF), na kusababisha kuhama mara moja kwa zaidi ya watu milioni 3.3, wakiwemo wakimbizi wa ndani (IDPs), wanaotafuta hifadhi na wakimbizi.
Mzozo huo uliendelea kuwa moja ya mapigano marefu na mabaya zaidi barani Afrika huku takwimu za vifo zikiongezeka siku baada ya siku. Hadi kufikia mwezi Disemba, zaidi ya watu 12,000 wameuawa katika mapigano hayo huku wengine milioni 8 wakiwa wameachwa bila makao.
Juhudi za upatanishi zimeshindikana mara kwa mara lakini mazungumzo bado yanaendelea huku kukiwa na wito wa kusitisha mapigano mara moja.
Jamhuri ya Kidemorasia ya Congo
Lakini unyo kwa unyo inafuata Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Nchi hiyo tajiri kwa madini itapiga kura mnamo Desemba 20 huku kukiwa na hofu ya kuendelea kwa ghasia hasa Mashariki mwa nchi, ambazo huenda zikavuruga mchakato wa upigaji kura.
Kufikia sasa takriban watu milioni 7.9 wamekimbia makazi yao ama kwa ndani au kama wakimbizi katika nchi jirani. Tangu kupata uhuru mwaka 1960, DRC imekumbwa na ghasia za makundi ya waasi.
Mnamo mwaka wa 2022, kuongezeka kwa ghasia katika majimbo ya Mashariki ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini kulizidisha hali ya ukosefu wa usalama nchini DRC, na kusababisha watu wengi kuhama makazi yao na kupoteza maisha.
Zaidi ya makundi 100 ya wapiganaji wamepiga kambi katika nchi hiyo kubwa wakipigania udhibiti wa migodi na maliasili za nchi hiyo.
Serikali zilizopita zimepata mafanikio kidogo au hazijapata mafanikio yoyote katika kunyang'anya silaha vikundi.
Ethiopia
Ingawa bado imeorodheshwa kuwa miongoni mwa nchi zenye mizozo barani Afrika, Ethiopia hivi karibuni imeonyesha kupungua kwa watu waliokimbia makazi yao ndani na nje ya nchi. Kufikia mwisho wa mwaka 2022 takriban watu milioni 1.8 walikuwa wamehamishwa kutokana na mizozo ya ndani katika eneo la Tigray.
Lakini mpango wa kusitisha mapigano ulileta matumaini pamoja na kupungua kwa mivutano katika maeneo mengine kama eneo la Oromia na kusababisha takriban Waethiopia milioni 1.2 kurejea makwao.
Hata hivyo ripoti za hivi punde za mapigano mapya huko Tigray na ukosefu wa data za kutosha kutoka eneo hilo huacha takwimu zisizo sahihi.
Nchi nyingine zilizokabiliwa na ukosefu wa usalama wa ndani na kuchangia idadi ya watu waliokimbia makazi yao ni Somalia, Nigeria, Cameroun, Burkina Faso, CAR, Mali, Chad na Niger.
Mabadiliko ya nguvu ya utawala
Kurejelea maelezo ya pale mwanzo. Wakati nchi za Afrika zikifanya uchaguzi, mabadiliko ya utawala ni mojawapo ya masuala nyeti ambayo yametikisa kiini cha demokrasia katika bara hilo.
Lakini habari za uasi wa askari mitaani sio za kushtua tena kama vile ungetarajia.
Katika kipindi cha miaka 3 iliyopita angalau mapinduzi 7 yamefanyika Afrika Magharibi huku Gabon ikiwa nchi ya punde zaidi mwishoni mwa Agosti.
Hii ilifuatia mapinduzi mengine yaliyofaulu nchini Niger mwezi mmoja kabla. Wanajeshi hao walisema walimpindua rais Mohamed Bazoum, ambaye alichaguliwa miaka miwili iliyopita katika makabidhiano ya kwanza ya amani na ya kidemokrasia ya Niger ya mamlaka tangu uhuru kutoka kwa Ufaransa, kwa sababu hakuweza kulilinda taifa kutokana na uasi unaoongezeka.
Watawala wa junta wamekuwa kwenye diplomasia ya kujaribu kukubalika ulimwenguni.
Hata hivyo, hadi sasa serikali nyengine za mapinduzi katika eneo hilo zimeikaribisha.
Mapinduzi mengine ya kijeshi yalikuwa Burkina Faso mnamo 2022; Chad, Guinea, na Sudan mwaka 2021 na Mali mnamo 2020.
Matukio haya pia yalichangia rekodi za migogoro katika bara ingawa nyingi za nchi hizo ziliepuka idadi kubwa ya wakimbizi.
Hii inaweza kuwa ni kutokana na ukweli kwamba mengi ya mapinduzi ya Afrika Magharibi yalipata uungwaji mkono kutoka kwa watu wao.
Kwa kuongezeka kwa idadi ya kupinduliwa kwa serikali na jeshi, hitaji la demokrasia ya wazi linahisi kuwa na nguvu zaidi kuwapa watu imani kwa viongozi wao. Nchi zisizopungua 18 zaidi ziko tayari kufanya uchaguzi wao mwaka wa 2024.
Je, hii itapunguza migogoro ya ndani ya bara? Je, uchaguzi wa watu utaheshimiwa na kudumishwa kwa muda wote?
Muda utasema.