Taarifa ya Sudan Return Monitoring Snapshot ilirekodi kurejea kwa watu hao kati ya Novemba 2024 na Septemba 2025, huku familia zikihama kutoka maeneo mengine ya nchi na hata kutoka mataifa ya nje.
"Kiwango cha watu kurejea Khartoum ni ishara ya uhimilivu wa watu, lakini pia ni onyo," alisema Ugochi Daniels, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Operesheni wa IOM, katika taarifa yake.
"Nilikutana na watu wanaorejea katika jiji ambalo bado lina athari za vita – nyumba zimeharibiwa na huduma za msingi hazifanyi kazi ipasavyo. Uamuzi wao wa kuanza upya ni wa kushangaza, licha ya kuwa maisha bado ni hatarishi sana."
Mwezi Machi, jeshi la Sudan lilidai kuwa limewafurusha wapiganaji wa Kikosi cha RSF kutoka Khartoum, takriban miaka miwili baada ya kupoteza udhibiti wa mji huo kwa kundi hilo la wanamgambo.
Mapigano kati ya jeshi na RSF yalianza mwezi Aprili 2023, na yamesababisha vifo vya maelfu ya watu.
Msaada wa kujenga upya
Khartoum bado ni makazi ya watu zaidi ya milioni 3.7 waliopoteza makazi yao, na wale waliorejea hadi sasa ni asilimia 26 tu ya jumla hiyo, kwa mujibu wa shirila la IOM.
Shirika hilo linakadiria kuwa watu milioni 2.7 zaidi wanaweza kurejea baadaye, kutegemea na hali ya usalama na misaada ya kibinadamu.
Nchini Sudan, watu milioni 2.6 wameweza kurejea katika maeneo yao ya awali tangu mwishoni mwa 2024, wakiwemo zaidi ya nusu milioni waliokuwa uhamishoni nje ya nchi, hasa kutoka Misri, Sudan Kusini, na Libya.
IOM imeonya kuwa wengi wa waliorejea wanaishi katika nyumba zilizoharibika au makazi yenye msongamano mkubwa, huku wakiwa na upungufu mkubwa wa maji safi, huduma za afya, au ulinzi. Magonjwa kama kipindupindu na malaria yanaendelea kuenea.
Shirika hilo limeitaka jumuiya ya kimataifa kuongeza misaada ya kujenga upya na kusaidia kurejesha huduma muhimu kwa jamii.