Rais wa mpito wa Madagaska Kanali Michael Randrianirina alimteua Herintsalama Rajaonarivelo kuwa waziri mkuu wa taifa hilo siku ya Jumatatu wakati wa hafla rasmi katika Ikulu ya Jimbo la Iavoloha.
Randrianirina alisema uteuzi wa Rajaonarivelo ulifanywa kufuatia pendekezo la wajumbe wa Bunge la Kitaifa.
"Alichaguliwa kwa ujuzi wake, uzoefu, na uhusiano na mashirika ya kimataifa," alisema.
Rajaonarivelo alichukua nafasi ya Zafisambo Ruphin Fortunat, aliyeteuliwa na Rais wa zamani Andry Rajoelina mnamo Oktoba 6, kufuatia kuvunjwa kwa serikali mnamo Septemba 29.
Rajaonarivelo, asiyejulikana sana katika ulingo wa kisiasa, alishikilia nyadhifa kadhaa za juu katika sekta ya kibinafsi, ikiwa ni pamoja na kuwa mwenyekiti wa zamani wa bodi ya wakurugenzi ya Benki ya BNI Madagascar.
Akiwa na shahada ya uzamili katika uchumi wa viwanda na uchumi wa biashara, Rajaonarivelo alikuwa mshauri wa kimataifa wa mashirika kadhaa ya kimataifa kama vile Benki ya Dunia, EU, Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, na Tume ya Bahari ya Hindi.
Aliongoza Chama cha Wafanyakazi wa Malagasi na kuchangia maendeleo ya miradi kadhaa inayoungwa mkono na washirika wa kimataifa kwa manufaa ya serikali ya Madagascar.
Rais Randrianirina aliapishwa kuwa rais siku ya Ijumaa kufuatia siku kadhaa za maandamano dhidi ya serikali ya Rais aliyeondolewa madarakani Rajoelina.
Maandamano yaliyoongozwa na vijana yalizuka Septemba 25 kutokana na uhaba mkubwa wa maji na umeme, pamoja na madai ya rushwa, baadaye yaligeuka haraka kuwa wito wa kumtaka aliyekuwa rais wa nchi hiyo Rajoelina kujiuzulu.
Kuna ripoti kwamba Rajoelina alihamishwa hadi Ufaransa kwa ndege ya kijeshi baada ya kufikia makubaliano na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.
Jumanne iliyopita kitengo cha kijeshi maalum kikiongozwa na Randrianirina kiliingia katika ikulu ya rais katika mji mkuu Antananarivo na kutangaza kuwa wamechukua mamlaka.
Mahakama Kuu ya Kikatiba nchini humo imemtaka Randrianirina kufanya uchaguzi ndani ya siku 60, kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo, ambayo inalazimu kufanywa uchaguzi wa urais ndani ya siku 30 hadi 60 baada ya mahakama kutangaza kuwa ofisi ya rais haina mtu.
Mahakama hio imesema Rajoelina hawezi kutimiza wajibu wake kwa vile hayupo nchini.