AFRIKA
1 dk kusoma
Raila Odinga ashushwa kaburini kwa heshima ya kijeshi
Viongozi mbali mbali walishuhudia maziko ya Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya Raila Odinga yaliyosindikizwa kwa mizinga 17 na heshima kamili ya kijeshi.
Raila Odinga ashushwa kaburini kwa heshima ya kijeshi
Shughuli ya mazishi ya Raila Odinga imekamilika / Reuters
tokea masaa 9

Saa kumi na moja jioni kwa saa za Afrika Mashariki, maziko yalikamilika ya hayati Raila Odinga, kiongozi wa muda mrefu wa upinzani nchini Kenya aliyewahi kuhudumu kama Waziri Mkuu wa nchi hiyo.

Raila alizikwa kwa heshima kamili ya kijeshi, huku wanajeshi wakilibeba jeneza lake na kulishusha kaburini.

Viongozi mbali mbali wakiwemo Rais William Ruto, marais wastaafu Uhuru Kenyatta na Olusegun Obasanjo, na waakilishi wengine pamoja na mjane wake Ida Odinga familia, mawaziri magavana na maseneta, pamoja na wageni wengine waheshimiwa walipokezana muda wa kumwaga mchanga kaburini na kuweka maua pembeni mwa kaburi.

Ibada ya wafu iliongozwa na Askofu wa Anglikana wa Siaya, David Kodia.

‘‘Kwa jasho lako utajipatia chakula mpaka utakaporudi udongoni ulimotwaliwa; maana wewe ni mavumbi, na mavumbini utarudi.”

Maziko haya yanakamilisha siku kadhaa za shughuli mbali mbali za kitaifa kwa heshima ya Raila Odinga, tangu mwili wake uliporudishwa kutoka India alikofia.

Raila Odinga amefariki akiwa na umri wa miaka 80.

Wakenya wanaendelea na maombolezo ya kitaifa ya siku saba yaliyotangazwa na Rais Ruto kuanzia tarehe kumi na sita Oktoba.

CHANZO:TRT Afrika Swahili