Watu wasiopungua 63 wamepoteza maisha katika ajali iliyohusisha magari kadhaa kwenye barabara kuu magharibi mwa Uganda, polisi wamesema.
Tukio hilo lilitokea kwenye barabara ya Kampala-Gulu muda mfupi baada ya saa sita usiku, wakati mabasi mawili "yaligongana uso kwa uso wakati wa jaribio la kuyapita magari mengine," polisi walisema katika taarifa iliyochapishwa kwenye X siku ya Jumatano.
Dereva mmoja alijaribu kukwepa kugongana, lakini badala yake akasababisha "mlolongo wa ajali" uliosababisha angalau magari mengine manne "kupoteza mwelekeo na kupinduka mara kadhaa," taarifa hiyo ilisema.
"Kufuatia ajali hiyo, watu 63 walipoteza maisha, wote wakiwa ni abiria wa magari yaliyohusika, na wengine kadhaa walipata majeraha," polisi walisema.
Wale waliojeruhiwa walikimbizwa katika Hospitali ya Kiryandongo na vituo vingine vya afya vilivyo karibu, taarifa hiyo iliongeza, lakini haikutoa maelezo zaidi kuhusu idadi ya majeruhi au hali ya majeraha yao.