MICHEZO
2 DK KUSOMA
Côte d'Ivoire yasema iko tayari kuandaa Afcon maridadi 2024
Wenyeji wa Kombe la Mataifa bora Afrika Soka, Côte d'Ivoire wanasema kuwa makala ya kombe hilo haitashuhudia msiba kama ilivyokuwa Cameroon.
Côte d'Ivoire yasema iko tayari kuandaa Afcon maridadi 2024
Kombe la Afcon 2024 litaandaliwa Côte d'Ivoire kuanzia mwezi Januari. Picha: Mashirika mbalimbali / Others
20 Desemba 2023

Kulingana na waandaaji wa kombe la Afcon Côte d'Ivoire, kila kitu kiko shwari tayari kwa ngarambe hizo za Kombe la mataifa ya Afrika, Afcon 2023.

Wenyeji hao wamesema kuwa wana uhakika kuwa hatua zao za usalama zitazuia marudio ya janga ambalo lilileta sifa mbaya kwa toleo la 2021 huko Cameroon.

Hii ni baada ya watu wanane kufa na kadhaa kujeruhiwa vibaya kutokana na msongamano wakati mashabiki wa nyumbani walipokuwa wakijikusanya kutazama mechi ya timu 16 za mwisho kati ya wenyeji Cameroon na Comoros.

Mashindano hayo yataanza Januari 13 hadi Februari 11 huku Senegal ikitetea taji waliloshinda kwa mara ya kwanza baada ya kuishinda Misri kupitia penalti.

Côte d'Ivoire ndio mwenyeji wa Kombe la Afcon 2023 baada ya uamuzi wa Shirikisho la Soka La Afrika (CAF) kuahirisha kutoka tarehe ya awali ya Julai hadi katika msimu wa joto kwa sababu ya hofu juu ya mechi hizo kuandaliwa wakati wa msimu wa mvua.

Youssouf Kouyate, mkurugenzi mkuu wa polisi nchini Ivory Coast, ameiambia AFP kuwa hatua zote zimechukuliwa kwa ajili ya viwanja vyote sita ili kuepuka mkasa kama huo- na waandaaji wanatarajia mashabiki milioni 1.5 kutoka nje ya nchi.

Kutakuwa na jumla ya askari na polisi wapatao 17,000 waliotumwa kwa ajili ya mashindano hayo na wafanyakazi 2,500 kwenye viwanja vya soka.

Ingawa Côte d'Ivoire ni mojawapo ya mataifa tajika soka barani Afrika, hata hivyo, hii itakuwa mara yao ya pili tu kuwa mwenyeji wa fainali hizo, baada ya 1984 wakati mashindano hayo yalijumuisha timu nane tu badala ya 24 zitakazoshiriki wakati huu.

CHANZO:AFP