| Swahili
AFRIKA
2 DK KUSOMA
Somalia iko tayari kudumisha mtangamano wa Afrika Mashariki
Kulingana na Katibu Mkuu wa Afrika Mashariki, Somalia imeonesha nia thabiti ya kudumisha mtangamano huo.
Somalia iko tayari kudumisha mtangamano wa Afrika Mashariki
Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud (kushoto) akipongezwa na  Rais Salva Kiir Mayardit wa Sudan ya Kusini mara baada ya Somalia kuidhinishwa kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki./Picha: Wengine / Others

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Veronica Mueni Nduva amesisitiza nia ya Jamhuri ya Shirikisho la Somalia katika kudumisha mtangamano wa jumuiya hiyo.

Akizungumza katika kikao cha wiki moja kinachoangazia mtangano wa EAC mjini Nairobi nchini Kenya, Nduva aliweka msisitizo kwenye muktadha wa kihistoria wa nchi ya Somalia unaliweka taifa hilo kwenye safari ya kuelekea na kufikia mtangamano wa Jumuiya hiyo yenye nchi wanachama nane.

"Jamhuri ya Shirikisho la Somalia ilipata kuwa mwanachama kamili wa EAC Machi 2024, baada ya kuwasilisha rasmi hati yake ya kuridhia Mkataba wa Kujiunga na Jumuiya hii, mkutano wa leo unaashiria hatua muhimu katika safari hii, kuoanisha michakato ya kitaifa ya Somalia na mifumo ya kikanda ili kuhakikisha ushirikiano wa kina,” alisema.

Kulingana na Nduva, mchakato huo utahusisha shughuli zinazopaswa kufanywa kwa pamoja kati ya Somalia na Mashirika na taasisi za EAC.

"Mchakato huu unaelezea shughuli muhimu zilizoainishwa katika mipango ya kitaifa na yenye mwelekeo wa jamii. Hizi ni pamoja na kuoanisha mfumo wa kisheria wa Somalia na viwango vilivyowekwa vya kikanda na kuhakikisha ushiriki thabiti katika programu na shughuli za EAC," aliongeza.

Kulingana na Nduva, hadi kukamilika kwake, mchakato huo utatumika kama nyenzo ya kimkakati ya kusawazisha programu na kukusanya rasilimali kwa ufanisi katika Jumuiya nzima.

Mwezi Mei, 2024, Somalia iliwasilisha hati ya idhini ya Mkataba wa Kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa katibu mkuu wa jumuiya hiyo katika makao makuu yake mjini Arusha, Tanzania, na kuifanya nchi hiyo kuwa mwanachama rasmi wa nane wa jumuiya hiyo ya kikanda.

Pata habari zaidi kupitia whatsapp channels

CHANZO:TRT Afrika