AFRIKA
2 dk kusoma
Watanzania wafanya maamuzi kupitia sanduku la kura
Uchaguzi Mkuu nchini Tanzania hufanyika kila baada ya miaka mitano kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano, Wabunge na Madiwani kwa upande wa Tanzania Bara. Zanzibar watakuwa na nyongeza ya kuchagua Rais wa visiwa hivyo na Wawakilishi.
Watanzania wafanya maamuzi kupitia sanduku la kura
Tanzania Election / AP
tokea masaa 15

Na Edward Josaphat Qorro akiwa Dodoma

Watanzania kutoka sehemu mbalimbali za nchi wameanza kupiga kura mapema hii. Zoezi hilo limeanza rasmi saa moja asubuhi na linatarajiwa kukamilika saa kumi alasiri.

TRT Afrika, ambayo imekita kambi jijini Dodoma imeshuhudia zoezi hilo likiendelea kwa utulivu, ingawa mwitikio unaonekana kuwa mdogo ikilinganishwa na uchaguzi uliopita. Tume ya uchaguzi nchini humo inatarajia wapiga kura milioni 37 kujitokeza na kuchagua viongozi wao katika ngazi ya urais, ubunge na udiwani.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza asubuhi hii na kufanikiwa kupiga kura ni Mohammed Yassin Aziz mkazi wa Dodoma ambae anasema kuwa amefurahi kufanikiwa kupiga kura. "Zoezi limeenda vizuri bila bughudha yoyote. Hii ni mara yangu ya nne kupiga kura. Kwa sasa hivi mwitikio sio mzuri tofauti na uchaguzi uliopita ambapo foleni zingekuwa ndefu zaidi," anasema Mohammed.

Hata hivyo, kwa Emmanuel Elias ambae aliwahi kufika katika kituo cha Jumba la Maendeleo kituo namba tatu kilichopo katika Kata ya Uhuru, Dodoma mjini baada ya kushindwa kupiga kura kutokana na taarifa zake kutokuwepo. Nimekuja kupiga kura kwa sababu ni haki yangu, Ila nimejisikia vibaya jina kukosekana, ila bado nina matumaini," anasema Emmanuel.

Kwa Asia Juma Abdallah siku hii amekuwa akiisubiri kwa hamu kwani anasema kuwa amefurahishwa kuona wanawake wengi wameshiriki katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa mwaka huu."Mimi ni mzalendo nimeamka asubuhi na mapema kuja kumchagua nimtakae. Hakuna usumbufu wowote uliojitokeza.

Ninaipongeza Tume ya Uchaguzi kwa maandalizi mazuri yaliyofanyika," amesema Asia pindi alipozungumza na TRT Afrika.Uchaguzi Mkuu nchini Tanzania hufanyika kila baada ya miaka mitano kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano, Wabunge na Madiwani kwa upande wa Tanzania Bara. Zanzibar watakuwa na nyongeza ya kuchagua Rais wa visiwa hivyo na Wawakilishi.

CHANZO:TRT Swahili