Shirikisho la Soka la Morocco (FRMF) limetangaza Jumanne kuwa litachukua hatua za kisheria kupinga uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) wa kuirejeshea Senegal ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025.
Katika taarifa yake, Shirikisho hilo la Morocco limedai kuwa mmoja wa waamuzi wa CAS, Ulrich Haas, aliwasiliana na Rais wa Shirikisho la Soka la Senegal (FSF), Abdoulaye Fall, saa 48 kabla ya kutolewa kwa uamuzi huo. Morocco imesema hali hiyo imeibua maswali kuhusu uadilifu na uhuru wa mchakato wa usuluhishi.
Haas alikuwa miongoni mwa waamuzi watatu wa jopo la CAS lililosikiliza rufaa ya Senegal dhidi ya uamuzi wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) wa kuipa Morocco utaji la AFCON.
Mapema Jumanne, Morocco iliripotiwa kuomba kutangazwa kwa hukumu hiyo kuahirishwa kutokana na madai ya kuwepo kwa mawasiliano hayo ya simu. Hata hivyo, vyanzo vilivyo karibu na Shirikisho la Soka la Senegal vilikanusha madai hayo, kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha Ufaransa, RMC Sport.
Shirikisho la Morocco pia limekosoa uamuzi huo kwa madai kwamba haukuzingatia kikamilifu msimamo wa hivi karibuni wa FIFA na Bodi ya Kimataifa ya Soka (IFAB) kuhusu wachezaji wanaoondoka uwanjani bila ruhusa ya mwamuzi na hatua za kinidhamu zinazopaswa kuchukuliwa.
Mapema Jumanne, CAS ilikubaliana kwa kauli moja na rufaa ya Senegal, na kubatilisha uamuzi wa CAF wa kuipa Morocco ushindi wa mabao 3-0 kufuatia fainali yenye utata iliyochezwa jijini Rabat Januari 18.
Uamuzi huo umeirejeshea Senegal ushindi wake wa awali wa bao 1-0 baada ya muda wa nyongeza.
CAS ilieleza kuwa mwamuzi wa mchezo ndiye aliyekuwa na mamlaka ya pekee ya kuamua mchezo kuendelea baada ya wachezaji wa Senegal kuondoka uwanjani kwa muda kupinga penalti iliyotolewa katika dakika za nyongeza za kipindi cha pili.










