Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imetangaza kuondoa hatua za muda zilizowekwa kurahisisha huduma za usafiri wa anga nchini, kuanzia Novemba 1, 2026.
Hatua hizo zilianzishwa Juni 18, 2025, kwa lengo la kuendeleza muunganiko wa safari za anga na kupunguza usumbufu kwa abiria na wadau wa sekta hiyo.
Miongoni mwa hatua hizo ni kuruhusu mashirika ya ndege ya kimataifa kupata haki za ziada za usafiri wa anga, pamoja na kutoa unafuu wa kiudhibiti kwa mashirika ya ndege ya Tanzania kupitia mikataba ya codeshare na vibali maalumu vya muda.
Katika taarifa iliyotolewa Oktoba 15, 2026, TCAA imesema uamuzi huo umetokana na mabadiliko ya hali ya uendeshaji na kupungua kwa hitaji la kuendelea na utaratibu huo wa muda.
Kutokana na uamuzi huo, mashirika yote ya ndege yatakayoathirika yanatakiwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazotumika katika uendeshaji wa usafiri wa anga nchini Tanzania.






















