Nchi ya Niger imesema imeanzisha msako wa kuwatafuta watu wenye silaha waliohusika na mauaji ya wanajeshi wasiopungua 13, kufuatia shambulio lililotokea katika eneo la Tillaberi, magharibi mwa nchi hiyo.
Katika taarifa iliyosomwa kupitia televisheni ya taifa, Wizara ya Ulinzi ya Niger ilisema kuwa kikosi cha Walinzi wa Taifa kilishambuliwa katika tukio lililoelezwa kuwa ni “shambulio la kigaidi lililofanywa na kundi kubwa la washambuliaji waliokuwa na silaha nzito.”
Nchi hiyo imekuwa ikikabiliwa na mashambulizi ya makundi yenye silaha yanayohusishwa na mtandao wa al-Qaeda na kundi la ISIL (Daesh), huku maelfu ya watu wakiuawa katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.
Kwa mujibu wa takwimu za awali zilizotolewa na Wizara ya Ulinzi, katika shambulio lililotokea Alhamisi katika kijiji cha Sanam, walinzi wasiopungua 13 waliuawa na wengine 20 kujeruhiwa.
Operesheni za kupambana na ugaidi
Walinzi waliolengwa katika shambulio hilo walikuwa sehemu ya operesheni maalumu ya kupambana na ugaidi.
Niger inaendelea kukabiliwa na hali ya ukosefu wa usalama katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo, kutokana na shughuli za makundi yenye silaha, mitandao ya uhalifu na biashara haramu katika mipaka ya nchi hiyo.
Mara kwa mara, vikosi vya usalama nchini humo hufanya operesheni zinazolenga kuvunja mitandao ya wapiganaji, kudhibiti njia za usambazaji wa vifaa na mahitaji ya kijeshi, pamoja na kupunguza shughuli za magendo, hususan katika maeneo ya mpakani na kandokando ya mito.
Katika miaka ya hivi karibuni, mamlaka zimeongeza operesheni za pamoja katika maeneo mbalimbali ya nchi, zikilenga kukabiliana na uvamizi wa makundi yenye silaha, biashara haramu ya mafuta na usambazaji wa silaha pamoja na vifaa vya vilipuzi.
Operesheni za kijeshi zilizofanyika hivi karibuni zinaonesha juhudi zinazoendelea za mamlaka za Niger za kudhibiti shughuli za mitandao inayoshukiwa kujihusisha na uasi wa kutumia silaha na uhalifu katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.














