| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Rais wa Kenya ataka uhalifu wa kupangwa kuchunguzwa zaidi
Wahitimu zaidi ya 350 walitunukiwa diploma, shahada na shahada za uzamili katika fani  mbalimbali za kitaaluma katika Chuo Kikuu cha Ulinzi cha Kitaifa.
Rais wa Kenya ataka uhalifu wa kupangwa kuchunguzwa zaidi
Rais wa Kenya William Ruto akiwa Chuo Kikuu cha Ulinzi cha Kitaifa - Kenya (NDU-K), Nakuru Kenya/Picha: Ikulu Kenya / Ikulu Kenya
 

Rais wa Kenya William Ruto amekipa Chuo Kikuu cha Ulinzi cha Kitaifa - Kenya (NDU-K) jukumu la kuchunguza sababu za ongezeko la uhalifu wa kupangwa katika sekta mbalimbali.

Rais Ruto ametoa agizo hilo alipokuwa akiongoza mahafali ya nne ya Chuo hicho katika Kaunti ya Nakuru.

“Naelekeza Chuo Kikuu, kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kitaifa ya Kupambana na Matumizi Mabaya ya Pombe na Dawa za Kulevya, Idara ya Usalama wa Taifa, na Wizara ya Mambo ya Ndani, kufanya utafiti wa kina kuhusu uchumi wa kisiasa wa pombe haramu na dawa za kulevya,” Rais alisema.

“Ni lazima tuelewe jinsi mitandao hii inavyofanya kazi, jinsi inavyofadhiliwa, jinsi inavyochochea uhalifu uliopangwa, na jinsi inavyoendeleza tatizo la matumizi mabaya ya dawa za kulevya na pombe,” alisisitiza.

Chuo Kikuu cha Ulinzi cha Kitaifa - Kenya (NDU-K) ni Chuo Kikuu cha umma, kilichoanzishwa mwaka 2021, lengo lake likiwa ni kutoa elimu ya juu, mafunzo, na kufanya utafiti katika nyanja za usalama wa taifa, ulinzi, na masomo ya kimkakati.

“Ninalipa Chuo Kikuu jukumu la kuchunguza moto wa mara kwa mara katika maeneo ya makazi duni na masoko mengine yasiyo rasmi ambayo huharibu biashara na kuwafukuza wafanyabiashara,” Rais aliagiza.

“Tunahitaji majibu yanayotokana na ushahidi wa kisayansi. Je, moto huu ni wa bahati mbaya, matokeo ya miundombinu isiyotosheleza ya usalama, au vitendo vya makusudi vya kuhujumu uchumi?”

Wahitimu zaidi ya 350 walitunukiwa diploma, shahada na shahada za uzamili, katika fani  mbalimbali za kitaaluma.

Wahitimu hao walijumuisha maafisa wa jeshi, watumishi wa serikali, na maafisa kutoka nchi washirika.

CHANZO:TRT Afrika Swahili