ULIMWENGU
2 dk kusoma
Trump ailalamikia Katiba ya Marekani kutomruhusu kuwania muhula wa tatu
Rais wa Marekani Donald Trump alieleza siku ya Jumatano kwamba hawezi kuwania muhula wa tatu, akisema Katiba ya Marekani haimruhusu kufanya hivyo.
Trump ailalamikia Katiba ya Marekani kutomruhusu kuwania muhula wa tatu
Katiba ya Marekani inamruhusu Rais kuongoza kwa muhula miwili pekee. / / Reuters
tokea masaa 4

Trump na wafuasi wake wamekuwa wakirudia mara kwa mara uwezekano wake wa kuwania urais mwaka wa 2028, jambo linalosababisha wasiwasi kwa wapinzani wake na furaha kwa wafuasi wake.

“Ninafanya vizuri zaidi katika kura za maoni, hata hivyo kutokana na yanayosemwa, naamini siwezi kuwania muhula wa tatu. Tutaona itakavyokuwa… Ni mbaya sana,” Trump alisema akiwa kwenye ndege ya Air Force One.

Katiba ya Marekani inamruhusu Rais kuongoza kwa muhula miwili pekee, na Trump alianza muhula wake wa pili Januari 20, 2025.

“Watu wengi wazuri”

Trump, aliyehudumu muhula wake wa kwanza kuanzia 2017 hadi 2021, mara nyingi husema wafuasi wake wanataka aendelee kuongoza licha ya kizuizi cha Katiba.

Hivi karibuni, Rais alionyesha kofia nyekundu zilizoandikwa “Trump 2028” kwenye dawati la Ofisi ya Ikulu.

Miongoni mwa wafuasi wake, wana hisia kubwa ya kwamba Makamu wa Rais JD Vance anaweza kuwania urais mwaka wa 2028 akiwa kwenye tiketi na Trump.

Trump alitangaza wiki hii kuwa wazo hilo haliwezekani na Jumatano alisema ni “dhahiri kabisa” kuwa hawezi kuwania tena. “Lakini tuna watu wengi wazuri,” alisema.

Hakuna njia ya kubadilisha Katiba

Spika wa Bunge, Mike Johnson, alisema Jumanne katika mkutano na waandishi wa habari Capitol kwamba alizungumza na Trump kuhusu kuwania muhula wa tatu lakini hajaona njia ya kufanya hivyo.

“Imekuwa kipindi kizuri, lakini nadhani rais anajua, na yeye na mimi tumezungumzia vikwazo vya Katiba,” Johnson alisema.

“Kuna Marekebisho ya 22,” Johnson aliongeza, akisema Katiba ni wazi, ingawa Trump hufurahia kuwatia mbwembwe wapinzani wake wa Demokratiki kwa kauli na kofia zilizoandikwa “Trump 2028”.

“Siwezi kuona njia ya kurekebisha Katiba kwa sababu inachukua takriban miaka 10,” Johnson alisema.

Atapata muhula wa tatu?

“Ungehitaji theluthi mbili za Bunge na robo tatu ya majimbo kuidhinisha,” Johnson alisema.

Mazungumzo kuhusu muhula wa tatu yalianza baada ya Steve Bannon, mshauri wa zamani wa Trump na mmoja wa wafuasi wake wakuu, kusema wiki iliyopita kwamba “kuna mpango” wa kumuweka White House.

“Atapata muhula wa tatu… Trump atakuwa rais mwaka wa 2028. Watu wanapaswa tu kukubali hilo,” Bannon alisema kwa kituo cha habari cha Marekani.

Akiulizwa kuhusu Marekebisho ya 22, ambayo yanakataza mihula zaidi ya miwili, Bannon alisema: “Kuna njia nyingi mbadala. Wakati unaofaa, tutaweka wazi mpango ulivyo.”

Hii si mara ya kwanza kwa mada ya kurudi kwa Trump kwa muhula wa tatu kuibuka. Mwezi Mei, Trump alibainisha uwezekano huo kwa wazi katika hotuba yenye siasa nyingi kwa wanajeshi wa Marekani huko Qatar.

 

 

CHANZO:AFP