UTURUKI
4 dk kusoma
Erdogan akamilisha ziara ya Ghuba, akitia saini mikataba 24 mipya na Kuwait, Qatar na Oman
Ziara ya siku tatu ya Rais wa Uturuki ililenga katika kuimarisha uhusiano wa pande mbili, ushirikiano wa kikanda, na kuunga mkono suluhisho la mataifa mawili katika Mashariki ya Kati.
Erdogan akamilisha ziara ya Ghuba, akitia saini mikataba 24 mipya na Kuwait, Qatar na Oman
Erdogan alitembelea nchi tatu za Ghuba Oktoba 21–23 kwa mwaliko wa viongozi wao. / / AA
tokea masaa 6

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, alihitimisha ziara yake ya siku tatu katika eneo la Ghuba siku ya Alhamisi, ambayo ilijumuisha ziara rasmi nchini Kuwait, Qatar na Oman, na kupelekea kutiwa saini kwa mikataba 24, hati za makubaliano na azimio la pamoja.

Ziara hiyo ya Erdogan katika nchi hizo tatu za Ghuba ilifanyika Oktoba 21–23 kwa mwaliko wa viongozi wao. Mazungumzo yote yalilenga kuimarisha uhusiano wa pande mbili na kupanua ushirikiano katika masuala ya kikanda na kimataifa, ikiwemo hali ya Gaza.

Kuwait

Erdogan alianza ziara yake nchini Kuwait, ambako Emir Meshal Al Ahmad Al Jaber Al Sabah alimkaribisha kwa sherehe rasmi katika Kasri la Bayan.

Viongozi hao wawili walifanya mazungumzo ya ana kwa ana pamoja na vikao vya pamoja vya wajumbe wao, ambapo walipitia uhusiano wa pande mbili na kubadilishana maoni kuhusu maendeleo ya kikanda na kimataifa.

Erdogan alisisitiza umuhimu wa kulinda makubaliano dhaifu ya kusitisha mapigano huko Gaza, akirudia msimamo wake kuwa suluhisho la mataifa mawili ndilo muhimu kwa amani ya kudumu. Alitoa wito wa umoja miongoni mwa mataifa ya Kiislamu na kuthibitisha utayari wa Uturuki kushirikiana na washirika wa Kiarabu kujenga mustakabali bora kwa Syria.

Baada ya mazungumzo hayo, Erdogan alimkabidhi Emir wa Kuwait gari la umeme aina ya Togg, lililotengenezwa nchini Uturuki.

Miongoni mwa makubaliano yaliyosainiwa ni pamoja na: Mkataba wa Usafiri wa Baharini, Makubaliano (MoU) kuhusu Utambuzi wa Vyeti vya Mabaharia, Makubaliano kuhusu Ushirikiano katika Nishati, na Makubaliano kuhusu Uhamasishaji wa Uwekezaji wa Moja kwa Moja kati ya Ofisi ya Uwekezaji ya Rais wa Uturuki na Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji wa Kuwait (KDIPA).

Baadaye, Emir wa Kuwait aliandaa chakula rasmi cha jioini kwa heshima ya Erdogan.

InayohusianaTRT Afrika - Erdogan amesisitiza umuhimu wa kudumisha usitishwaji vita Gaza katika mazungumzo na Amir wa Kuwait

Qatar

Baadaye Erdogan alisafiri hadi Doha, ambako alikaribishwa na sherehe rasmi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hamad kabla ya kukutana na Amiri wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani katika kasri la Amiri.

Mazungumzo yalilenga kuimarisha ushirikiano katika sekta ya ulinzi, biashara, nishati, na uwekezaji, pamoja na yanayojiri Palestina.

Erdogan alielezea uhusiano wa Uturuki-Qatar kama "bora," akisema ushirikiano wa kimkakati wa mataifa hayo mawili una nafasi muhimu katika utulivu wa kikanda.

Viongozi hao waliongoza kwa pamoja Mkutano wa 11 wa Kamati ya Juu wa Kimkakati Uturuki – Qatar, ambapo walitia saini mikataba mipya ya ushirikiano, ikijumuisha: Makubaliano ya Mpango wa Maendeleo ya Kimkakati, Makubaliano ya Ushirikiano wa Sekta ya Ulinzi, Azimio la Pamoja la Mkutano wa Kamati Kuu ya Kimkakati, na Taarifa ya Pamoja ya Mawaziri kati ya wizara za biashara za nchi hizo mbili.

Rais wa Uturuki pia alihudhuria chakula cha jioni kilichoandaliwa kwa heshima yake na amiri wa Qatar.

InayohusianaTRT Afrika - Erdogan awasili Qatar kwa mkutano na Amir Al Thani

Oman

Sehemu ya mwisho ya ziara ya Erdogan katika Ghuba ilikuwa jijini Muscat, Oman, ambako alipokelewa kwa heshima kamili na Sultani Haitham bin Tariq katika Kasri la Al Alam.

Viongozi hao wawili walijadili masuala ya pande mbili na ya kikanda, wakisisitiza mtazamo wao wa pamoja kuhusu suala la Palestina na umuhimu wa diplomasia inayojikita kwenye mazungumzo.

Erdogan alisifu nafasi ya Oman kama mpatanishi katika migogoro ya kikanda na kusema kuwa Uturuki na Oman zitaendelea kuunga mkono juhudi za kufanikisha suluhisho la mataifa mawili huko Gaza.

Erdogan alimkabidhi Sultani Haitham gari jekundu la umeme aina ya Togg kabla ya kushuhudia hafla ya kusaini makubaliano yanayogusa maeneo mbalimbali kama ulinzi, nishati, madini, viwanda, elimu ya juu, vyombo vya habari na masuala ya viza.

Miongoni mwa mikataba yaliyosainiwa ni:

Mkataba kuhusu Madini Muhimu, Mkataba wa Ushirikiano wa Kijeshi, Mkataba wa Ushirikiano wa Viwanda, Mkataba wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu, Mktaba wa Ulinzi wa Ushindani katika Soko, Mkataba kuhusu Vyombo vya Habari na Mawasiliano, Mkataba wa Ushirikiano katika Sekta ya Ulinzi, Mkataba wa Ushirikiano wa Kistratejia kati ya Mfuko wa Uturuki na Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman, pamoja na mikataba kadhaa ya umiliki wa hisa na ushirikiano kati ya kampuni za Uturuki na Oman, ikiwemo OYAK, Amber Limited, Uzbek-Oman Investment Company na Oman Food Investment Holding, Mkataba na Kampuni ya i ya Innovance Information Technologies Inc. na Kampuni ya Mawasiliano ya Oman, na Mkataba wa Ushirikiano wa Upatikanaji wa Sehemeu Ardhi kwa ajili ya Taasisi ya Maarif ya Uturuki kuanzisha shule nchini Oman.

Azimio ya pamoja pia yalisainiwa: moja kuhusu kuanzishwa kwa Baraza la Uratibu na jingine kuhusu msamaha wa viza kwa wamiliki wa pasipoti za kawaida.

Baada ya kushiriki chakula cha mchana kilichoandaliwa na Sultani Haitham, Erdogan aliondoka Muscat na kurejea Uturuki, na hivyo kukamilisha ziara yake ya siku tatu ya Ghuba.

InayohusianaTRT Afrika - Erdogan na Sultan wa Oman wakutana Muscat, waahidi kuimarisha uhusiano, kuunga mkono Palestina

CHANZO:AA