Kwa nini Afrika inatakiwa kuwa na wasiwasi kuhusu uvamizi wa Trump Venezuela
AFRIKA
4 dk kusoma
Kwa nini Afrika inatakiwa kuwa na wasiwasi kuhusu uvamizi wa Trump VenezuelaWataalamu wanaonya kuwa hatua ya kijeshi ya Marekani nchini Venezuela inaweza kufungua njia ya kuhalalisha mashambulizi dhidi ya viongozi wa mataifa mengine ambayo yamewahi kuwa katika mvutano na utawala wa Rais Donald Trump.
Waandamanaji wamebeba picha ya Rais wa Venezuela Nicolas Maduro wakita wito wa kuachiliwa mara moja jijini Caracas, Venezuela. / / Reuters
7 Januari 2026

Na Emmanuel Oduor

Baada ya Marekani kumteka nyara Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro, na kuahidi kuhamasisha makampuni ya nishati ya Marekani kunufaika na utajiri wa mafuta wa nchi hiyo, wasiwasi umeongezeka kuhusu hatua ambazo Marekani inaweza kuchukua katika migogoro na mataifa ya Afrika.

Wataalamu wanasema kuwa hatua hiyo ya kijeshi ya Marekani nchini Venezuela inaweza kuwa ni mfano hatari wa mashambulizi dhidi ya viongozi wa mataifa mengine ambayo yamekuwa na migogoro na serikali ya Rais Donald Trump.

Mataifa ya Afrika pamoja na mashirika ya kikanda barani humo yameshtumu operesheni hiyo ya kushtukiza dhidi ya rais wa Venezuela — ambaye mawasiliano yake ya mwisho hadharani na kiongozi wa Afrika yalikuwa mkutano na Rais wa Burkina Faso, Ibrahim Traore, mjini Moscow wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ushindi ya Urusi mnamo Mei 2025.

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, alieleza hatua ya kijeshi ya Marekani nchini Venezuela kama onyo kwa Waafrika kuyapa kipaumbele masuala ya usalama wa kimkakati ili kulinda bara lao ardhini, baharini, na ulinzi wa angani. Aliwaonya viongozi wa Afrika dhidi ya kutaka kubaki kuwa “samaki wakubwa kwenye mabwawa madogo”.

“Watu wengine hupenda hali hiyo ya kuwa samaki mkubwa kwenye bwawa dogo. Unajiona mkubwa sana, lakini matatizo yakitokea, huenda usiokoke,” alisema wakati wa mkutano na waandishi wa habari alipoulizwa kuhusu mafunzo ambayo Afrika inaweza kujifunza kutokana na yaliyojiri Venezuela.

Trump tayari amekuwa akiishambulia Nigeria kwa madai yasiyo na msingi ya “mauaji ya Wakristo” na kuitaja kama “Nchi yenye kumtia wasiwasi”. Mwezi uliopita aliidhinisha mashambulizi ya anga dhidi ya maeneo ya Daesh kaskazini-magharibi mwa Nigeria, akidai kundi hilo limekuwa likiwalenga Wakristo.

Marekani pia imeiwekea Afrika Kusini ushuru mkubwa wa kibiashara kutokana na madai ya “mauaji ya wazungu” — ambayo hayana msingi yanayodai kuwa kuna kampeni nchini humo ya kuwaua wakulima wazungu na kuwanyang’anya ardhi yao.

“Taifa linatakiwa kulaani na kukemea kilichotokea (Venezuela) kama ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa. Ni muhimu kufanya hivyo ili kuepusha kuwepo kwa mfano mbaya na kufikisha ujumbe kwa Trump, na pia kwa nchi nyingine, kwamba tabia kama hiyo haikubaliki na haitavumiliwa na dunia,” alisema Yusra Suedi, mhadhiri wa Sheria za Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Manchester, alipozungumza na TRT Afrika.

Wataalamu wanaeleza kuwa sheria za kimataifa haziruhusu taifa kumkamata kiongozi wa nchi huru isipokuwa kwa kujilinda au kwa idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

“Venezuela haikushambulia Marekani, wala haikuwa inapanga kuishambulia. Kwa kweli, Maduro alikuwa amesema yuko tayari kufanya mazungumzo na Trump kuhusu biashara ya dawa za kulevya. Pia hakukuwa na idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, hivyo ni wazi kuwa kitendo hicho ni kinyume cha sheria,” Suedi alieleza.

“Hapa ndipo umuhimu wa nchi kusimama dhidi ya kile Trump amefanya kama kitendo haramu chini ya sheria za kimataifa,” aliongeza.

Umoja wa Afrika (AU) ulieleza “wasiwasi mkubwa” kuhusu hatua ya kijeshi ya Marekani nchini Venezuela. Ulisisitiza tena dhamira yake thabiti ya kuheshimu misingi ya sheria za kimataifa, ikiwemo kuheshimu uhuru wa mataifa, mipaka yao ya kieneo, na haki ya watu kujitawala, kama ilivyoainishwa katika Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) ilitoa wito wa “kuheshimu uhuru na mipaka ya eneo la Venezuela”. Ilikiri “haki ya mataifa kupambana na uhalifu wa kimataifa” lakini ikasisitiza umuhimu wa kuheshimu sheria za kimataifa.

Jumuiya hiyo ilieleza mshikamano wake na raia wa Venezuela, “wanapojenga mustakabali wa nchi yao kupitia mchakato wa ushirikiano,” ilisema katika taarifa yake.

Afrika Kusini ilichukua msimamo mkali, ikiituhumu Marekani kwa kukiuka wazi Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

“Historia imeonesha mara kwa mara kuwa uvamizi wa kijeshi dhidi ya mataifa huru husababisha machafuko na kuongeza migogoro. Matumizi ya nguvu yasiyo halali na ya upande mmoja kwa namna hii yanadhoofisha uthabiti wa mfumo wa kimataifa na kanuni ya usawa kati ya mataifa,” ilisema taarifa kutoka wizara yake ya mambo ya nje.

Ghana ilieleza “kutoridhishwa kwake dhidi ya matumizi ya nguvu ya upande mmoja”, huku Chad ikisisitiza “umuhimu wa kulinda amani, utulivu na mipaka ya eneo la Venezuela”.

Je, hatua ya Trump ilikuwa halali?

Rais Trump alitetea utekaji wa rais wa Venezuela kwa madai ya uhusiano na biashara ya dawa za kulevya na ushirikiano na magenge ya wauza dawa, ingawa wataalamu wa sheria za kimataifa wanaona hoja hiyo haina msingi.

“Chini ya sheria za kimataifa, taifa haliwezi kuhalalisha uvunjaji wa sheria za kimataifa kwa kutegemea sheria zake za ndani. Hivyo, hata kama maafisa fulani wa Marekani wataona kitendo hiki kuwa halali chini ya sheria za Marekani, hilo haliondoi wajibu wa kimataifa wala halihalalishi au kufumbia macho kile ambacho serikali ya Trump imefanya kwa mujibu wa sheria za kimataifa,” Suedi alisisitiza.

 

CHANZO:TRT Afrika
Soma zaidi
Mshambuliaji wa Algeria awaomba radhi mashabiki wa DRC
Rais Touadera amualika Putin wa Urusi kutembelea Jamhuri ya Afrika ya Kati
Waziri wa zamani wa sheria Nigeria Malami apewa dhamana katika kesi ya fedha zilizoibwa
Trump aongeza Uganda, na mataifa mengine 11 ya Afrika kwenye orodha ya dhamana ya viza ya Marekani
Umoja wa Afrika waitaka Israel kubatilisha utambuzi wa Somaliland
Jeshi la Benin lawaua 'magaidi' 45 kaskazini mwa nchi
Nchi za Afrika zaunga mkono Venezuela baada ya operesheni ya kijeshi ya Marekani iliyomlenga Maduro
Somalia yashtumu ziara ya waziri wa mambo ya nje wa Israel Somaliland, ikiitaja kama ‘uvamizi’
Mahakama ya Tunisia yawaachilia huru wafanyakazi wa NGO waliokamatwa kwa kuwasaidia wahamiaji
Baraza la Makanisa nchini Kenya lajitenga na mhubiri anayedai miujiza 'Nabii Owour'
Misri imepokea watalii milioni 19 mwaka 2025: Waziri
Rais Touadera achaguliwa tena kuwa rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati
Washukiwa wa ugaidi washambulia mgodi wa dhahabu, wawateka wafanyakazi nchini Mali
Vita vya Sahel na changamoto za makundi ya kigaidi
Tanzania yapiga marufuku wageni kutoa baadhi ya huduma katika sekta ya madini, kulinda wazawa
Mahakama Kuu ya Guinea yamthibitisha Doumbouya mshindi wa uchaguzi
Jeshi la Sudan lazuia shambulio la droni la RSF kwenye bwawa kuu na maeneo ya kijeshi
Rais William Ruto apendekeza adhabu ya kifo kwa wauzaji wa dawa za kulevya
Nigeria yaagiza msako mkali baada ya watu wenye silaha kufanya mauaji katika jimbo la Niger
Tanzania yaaga mashindano ya AFCON 2025