Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, atazuru Uturuki siku ya Ijumaa kwa mazungumzo na mwenzake wa Uturuki, Hakan Fidan, ambapo majirani hao wawili wanatarajiwa kuimarisha ushirikiano katika masuala ya usalama, biashara na migogoro mbalimbali ya kikanda, vyanzo vya Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki vimesema.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki anatarajiwa kueleza kuwa nchi yake inafuatilia kwa karibu yanayojiri nchini Iran na kwamba inaona usalama, amani na uthabiti wa Iran kuwa na umuhimu mkubwa kwa Uturuki.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, Fidan atasisitiza tena msimamo wa Uturuki wa kupinga uingiliaji wowote wa kijeshi dhidi ya Iran, akionya kuwa hatua hiyo inaweza kusababisha hatari kubwa za kikanda na kimataifa.
Pia atasisitiza utayari wa Uturuki kusaidia kupunguza mvutano uliopo kupitia mazungumzo na kuunga mkono suluhisho la haraka na la amani la suala la nyuklia la Tehran, na kwamba Uturuki iko tayari kutoa msaada iwapo utahitajika.
Uturuki inataka kupanua ushirikiano
Fidan pia anatarajiwa kusisitiza kuwa uhusiano kati ya Uturuki na Iran — nchi mbili zilizounganishwa na historia ndefu — ni muhimu kwa usalama, uthabiti na ustawi wa kikanda.
Aidha, atasisitiza nia ya Uturuki ya kuimarisha zaidi ushirikiano kupitia mifumo iliyopo kama vile Baraza la Ushirikiano wa Ngazi ya Juu kati ya Uturuki na Iran, lililoanzishwa mwaka 2014.
Moja ya mada kuu ya mazungumzo itakuwa kuongezeka kwa biashara ya mataifa hayo mawili kufikia lengo lililowekwa kwa muda mrefu la dola bilioni 30.
Fidan ataweke wazi maslahi ya Uturuki katika kupanua ushirikiano katika biashara, nishati, usafirishaji na muunganisho wa miundombinu, ikiwemo kupitia vituo vya biashara mpakani.
Ushirikiano dhidi ya makundi ya kigaidi
Ushirikiano wa kiusalama utapewa kipaumbele, ambapo Fidan anatarajiwa kuangazia matendo ya kundi la kigaidi PKK tawi la Iran, linalojulikana kama PJAK, katika mambo yanayojiri hivi karibuni, na kusisitiza haja ya dharura ya kulidhoofisha kabisa kundi hilo kwa ajili ya usalama wa Iran.
Migogoro ya kikanda nje ya Iran pia itajadiliwa. Fidan atasisitiza uungaji mkono wa Uturuki kwa mifumo inayohusiana na awamu ya pili ya mpango wa amani wa Gaza, akipa kipaumbele utekelezaji wa haraka wa hatua madhubuti, ikiwemo utoaji wa misaada ya kibinadamu ya kutosha bila ya kutatizwa.
Pia atasitiza msimamo wa Ankara wa kuunga mkono ujenzi upya wa Gaza kwa njia itakayowawezesha Wapalestina kubaki katika ardhi yao na kuishi kwa amani na usalama.
Fidan anatarajiwa kutoa wito kwa nchi za kikanda kushirikiana kwa mshikamano na ushirikiano ili kukabiliana na kile ambacho Uturuki inakiita hatua za Israel zinazodhoofisha uthabiti wa kikanda.
Amani na usalama nchini Syria
Kuhusu Syria, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki atamueleza mwenzake wa Iran ya kuwa kuimarisha amani na usalama nchini humo kutachangia uthabiti wa kikanda.
Atasisitiza umuhimu wa Makubaliano ya Kusitisha Mapigano na Ujumuishaji Kamili (Ceasefire and Full Integration Agreement) katika kulinda uhuru wa mipaka ya Syria, umoja na mamlaka yake, na kusisitiza umuhimu wa kudumisha usitishaji mapigano ili kuepuka kudhoofisha mapambano dhidi ya Daesh.
Uturuki na Iran zilifanya mkutano wa 8 wa Baraza la Ushirikiano wa Ngazi ya Juu mjini Ankara mwezi Januari 2024 chini ya uenyekiti wa pamoja wa Rais Recep Tayyip Erdogan na aliyekuwa Rais wa Iran, marehemu Ebrahim Raisi.
Rais Erdogan alikutana mara ya mwisho na Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, mwezi Septemba 2025 katika mkutano wa Shirika la Ushirikiano la Shanghai uliofanyika nchini China.
















