Dembele ndiye mshindi wa tuzo ya Ballon d’Or mwaka 2025.
Masour Ousmane Dembele mwenye umri wa miaka 28 anasemekana kuwa mmoja wa wachezaji kandanda bora duniani na alianza kupepeta gozi ya kulipwa akiwa na timu ya Rennes ya Ufaransa.
Mwaka 2016 alielekea Ujerumani kujiunga na Borussia Dortmund na msimu wake wa kwanza tayari akabeba ndoo ya Kombe la Ujerumani la DFB-Pokal.
2017 akatuwa pale Barcelona, huko hakukidhi kiu cha timu hiyo ya kaskazini mashariki mwa Hispania, lakini alifanikiwa kushinda mataji kadhaa na wababe hao ikiwemo Ligi Kuu ya La Liga mara tatu, Kombe la Copa del Rey mara mbili na mataji mawili ya Supercopa de Espana au ‘Super Cup’.
Mwaka 2023 Dembele alirejea Ufaransa na kujiunga na mabingwa mara 13 wa Ligi Kuu ya nchi hiyo PSG.
Msimu wa 2024-25 wa winga teleza Dembele uliimarika zaidi ikawa kama kurutubisha kipaji chake. Aliifungia timu yake magoli 33 na kusaidia kutoa pasi zilosababisha kupatikana kwa magoli 15 katika mechi 49 alizocheza PSG.
Alichaguliwa mchezaji bora wa mwaka wa Ligi Kuu ya Ufaransa Ligue 1 na mchezaji bora wa msimu wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya, pamoja na kumaliza msimu akiwa mfungaji bora.
Mafanikio haya yalimfanya ashinde tuzo ya juu katika soka ya Ballon d’Or mwaka 2025.
Masour Ousmane Dembele ni mzaliwa wa eneo la Vernon, Eure, kanda ya Normandy, Kaskazini mwa Ufaransa. Asili ya mama yake ni Mauritania na Senegal na baba yake mzazi ni wa asili ya kutoka nchi ya Mali.














