Chama Cha Mapinduzi (CCM) cha nchini Tanzania, kimewatangazia wanachama wake ambao ni wabunge wateule na wanachama nafasi za kuwania Uspika wa Unaibu Spika ndani ya Bunge la nchi hiyo.
Katika taarifa yake iliyotolewa na Katibu wake wa NEC anayeshughulikia Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenan Laban Kihongosi, chama hicho kimewataka wabunge wateule na wanachama wake wenye sifa kuwania nafasi hizo kwa kuchukua fomu katika Ofisi za Makao Makuu ya chama hicho jijini Dodoma, Ofisi ndogo Lumumba Dar es Salaam na Afisi Kuu Kisiwandui, visiwani Zanzibar.
Hali kadhalika, chama hicho kiliwatangazia wanachama wake wenye sifa, nafasi za kugombea Uspika na Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi kwa upande wa Zanzibar.
Kulingana na CCM, fomu hizo zinapaswa kurejeshwa kwenye ofisi tajwa siku ya Novemba 4, 2025, saa 10 jioni.
Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya kuapishwa wa Samia Suluhu Hassan kama rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kufuatia ushindi wake wa kiti hicho katika uchaguzi wa Oktoba 29, 2025.
Mara baada ya uapisho wake, Rais Samia alimteua Hamza Johari, kama Mwanasheria wa Serikali nchini Tanzania.








