Pape Thiaw alikuwa sehemu ya kikosi cha Senegal kilichoitupa nje Ufaransa ya akina Zinedine Zidane na Fabian Barthez, kufuatia bao lililotiwa kimiani na marehemu Papa Bouba Diop.
Kwa sasa, huyu ndiye shujaa wao wa Simba wa Teranga, baada ya kuwaongoza Senegal kutwaa ubingwa wa Kombe la AFCON, kwa kuifunga Morocco hivi karibuni.
Pape Bouna Thiaw amekuwa na timu hiyo tangu Disemba 13, 2024.
Alitwaa mikoba ya nyota mwenzake, Rastafarian Aliou Cisse, ambaye walikuwa wote dimbani wakati wanawaondoa akina Zidane.
Licha ya kuipa mafanikio Senegal, Pape Thiaw atakumbukwa kwa kitendo chake cha kutoa timu uwanjani, baada ya kuonekana dhahiri kutoridhishwa na maamuzi ya Jean-Jacques Ndala Ngambo wa DRC.
Kabla ya kutundika daluga, Thiaw amewahi kukiputa na vilabu mbalimbali vya nchini Ufaransa, Uswizi na Uhispania miongoni mwa ligi zingine.
Alizaliwa pale mji wa mishemishe nyingi, Dakar na anatarajia kufikia miaka 45, ifikapo mwezi Februari.
Mtaalamu huyo, ameichezea timu yake ya taifa jumla ya michezo 16, akitia nyavuni mabao 5 kwa Simba wa Teranga.
Mbali na mafanikio ya AFCON 2025, Pape Thiaw amekuwa chachu ya kufuzu kwa timu ya Senegal kwenye michuano ya Kombe la Dunia, baadae mwaka huu.
Wakiwa bado wanaogelea kwenye minoti na ploti za viwanja, je ataweza kuiongoza vyema Senegal licha ya kukabiliwa na rungu kutoka CAF?













