Ikulu ya Marekani ilitoa ufafanuzi Jumamosi kuhusu sera yake mpya ya viza ya H-1B ambayo ilikuwa imezua taharuki katika sekta ya teknolojia, ikisema ada ya dola 100,000 itakuwa malipo ya mara moja tu kwa waombaji wapya.
Waziri wa Biashara wa Marekani, Howard Lutnick, alipotangaza ongezeko kubwa la ada hiyo Ijumaa, alisema italipwa kila mwaka na itawahusu watu wanaotafuta viza mpya pamoja na wale wanaotaka kuongeza muda wa viza zao.
Hata hivyo, Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Karoline Leavitt, alitoa ufafanuzi Jumamosi, saa chache kabla ya sera hiyo mpya kuanza kutekelezwa.
"Hii sio ada ya kila mwaka. Ni ada ya mara moja tu ambayo inahusu viza mpya pekee, si kwa wale wanaohuisha viza zao wala wale walioko na viza tayari," alisema kupitia chapisho la mitandao ya kijamii.
Taharuki
Amri hiyo ya kiutendaji, ambayo huenda ikakabiliwa na changamoto za kisheria, inaanza kutekelezwa Jumapili saa 12:01 asubuhi kwa muda wa Mashariki wa Marekani (0401 GMT), au saa 3:01 usiku Jumamosi kwa muda wa Pwani ya Pasifiki.
Kabla ya ufafanuzi wa Ikulu, kampuni za Marekani zilikuwa zikihangaika kuelewa athari za sera hiyo kwa wafanyakazi wao wa kigeni, huku baadhi zikidaiwa kuwaonya wafanyakazi wao kutosafiri nje ya nchi.
Baadhi ya watu waliokuwa tayari kwenye ndege wakijiandaa kuondoka nchini Ijumaa walishuka kwa hofu kwamba huenda wasiruhusiwe kuingia tena Marekani, gazeti la San Francisco Chronicle liliripoti.
"Wale ambao tayari wana viza za H-1B na kwa sasa wako nje ya nchi hawatatozwa dola 100,000 ili kuingia tena," alisema Leavitt.
Inayotumika sana na sekta ya teknolojia
"Wamiliki wa viza za H-1B wanaweza kuondoka na kurudi nchini kwa kiwango kilekile kama kawaida," aliongeza.
Viza za H-1B huruhusu kampuni kudhamini wafanyakazi wa kigeni wenye ujuzi maalum – kama wanasayansi, wahandisi, na waprogramu wa kompyuta – kufanya kazi Marekani, awali kwa miaka mitatu lakini inaweza kuongezwa hadi miaka sita.
Viza hizi zinatumika sana na sekta ya teknolojia. Raia wa India wanachukua karibu robo tatu ya vibali vinavyotolewa kupitia mfumo wa bahati nasibu kila mwaka.
Marekani iliidhinisha takriban viza 400,000 za H-1B mwaka 2024, ambapo theluthi mbili zilikuwa ni za kuhuisha.
"Watalipa"
Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza mabadiliko hayo Washington Ijumaa, akisema yangeunga mkono wafanyakazi wa Marekani.
Mpango wa H-1B "umetumiwa vibaya kwa makusudi kuchukua nafasi ya wafanyakazi wa Marekani badala ya kuwaongezea, kwa kutumia wafanyakazi wa kigeni wanaolipwa mishahara midogo," amri ya kiutendaji ilisema.
Trump pia alianzisha mpango wa ukaazi wa "kadi ya dhahabu" wa dola milioni 1 ambao alikuwa ameutangaza miezi kadhaa iliyopita.
"Jambo kuu ni kwamba, tutakuwa na watu wazuri wanaokuja, na watakuwa wakilipa," Trump aliwaambia waandishi wa habari alipokuwa akisaini amri hizo katika Ofisi ya Oval.
"Je, mtu ni wa thamani ya kutosha?"
Lutnick, ambaye alijiunga na Trump katika Ofisi ya Oval, alisema mara kadhaa kwamba ada hiyo ingetumika kila mwaka.
"Kampuni inahitaji kuamua... je, mtu huyo ana thamani ya kutosha kulipia dola 100,000 kwa mwaka kwa serikali? Au wanapaswa kurudi nyumbani na waajiri Wamarekani," aliwaambia waandishi wa habari.
Ingawa alidai kuwa "kampuni zote kubwa ziko tayari," biashara nyingi zilibaki na mkanganyiko kuhusu maelezo ya amri ya H-1B.
Benki ya Marekani JPMorgan ilithibitisha kuwa ilituma memo kwa wafanyakazi wake wenye viza za H-1B ikiwashauri kubaki Marekani na kuepuka safari za kimataifa hadi mwongozo zaidi utakapopatikana.
Ukosefu wa vipaji vya ndani vya kutosha
Wajasiriamali wa teknolojia – akiwemo mshirika wa zamani wa Trump, Elon Musk – wameonya dhidi ya kulenga viza za H-1B, wakisema kuwa Marekani haina vipaji vya ndani vya kutosha kujaza nafasi muhimu za kazi katika sekta ya teknolojia.
Wizara ya Mambo ya Nje ya India ilisema uhamaji wa vipaji wenye ujuzi umechangia "ubunifu" na "utengenezaji wa mali" katika nchi zote mbili na kwamba itatathmini mabadiliko hayo.
Ilisema katika taarifa kuwa hatua hiyo mpya huenda ikawa na "athari za kibinadamu kwa njia ya usumbufu kwa familia," jambo ambalo ilitarajia mamlaka za Marekani zitalishughulikia.