Wakati viongozi wa nchi mbalimbali duniani wakikutana nchini Marekani kwa ajili ya Mkutano Mkuu wa 80 wa Umoja wa Mataifa, suala la Palestina tayari limechukua kipaumbele.
Ureno, Uingereza, Canada na Australia zimelitambua rasmi taifa la Palestina kabla ya mkutano huo Mkuu wa UN.
Ufaransa, Luxemburg, na Malta zilitangaza pia kuwa na mpango kama huo. Kufikia sasa, zaidi ya nchi 145 ambazo ni wanachama wa Umoja wa Mataifa wametambua hitaji la kuwepo rasmi kwa Taifa Huru la Palestina.
Lakini hii ina maana gani?
Umoja wa Mataifa umesema Israel imefanya mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.
Kutambuliwa kwa Palestina kunafungua njia ya uwezekano wa kukomesha mateso wanayopitia watu wa Gaza, ambapo Israel imeripotiwa kuwaua takriban Wapalestina 65,000 tangu Oktoba 2023 huku maelfu wakilazimishwa kuhama makazi yao.
Kuporomoka kwa sekta ya afya na kukosekama kwa misaada muhimu ikiwemo chakula kumesababisha hali ya kukata tamaa katika maisha ya Wapalestina.
Shinikizo la kimataifa dhidi ya Israel linalenga kusitishwa kwa mapigano Gaza na upatikanaji wa haraka wa huduma za kibinadamu kwa watu wa Gaza, na hatimaye uwezo wa Palestina kusimama kama taifa huru mbali na udhibiti wa Israel.
Uamuzi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1947, wa kutekeleza suluhu ya mataifa mawili haujawahi kutokea, ingawa ilijinyakulia ardhi na utawala wa nguvu ya watu wa Palestina. Wataalamu wanasema utambuzi wa maneno lazima ufuatwe na vitendo.
Kwa Palestina kupata kiti rasmi katika Umoja wa Mataifa hii inaweza tu kuidhinishwa na Baraza la Usalama ambapo nchi 5 zina mamlaka ya kura ya turufu.
Marekani, ambayo ni mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama na kura ya turufu, tayari imekataa wito wa kutambuliwa kwa wakati huu.
Wataalamu pia wanasema shinikizo la kukabiliana na nchi moja moja kama vile vikwazo, kusimamisha uhusiano wa kibiashara, kunaweza kuishinikiza Israel kuipa Palestina uhuru wake. Afrika pia imekuwa sehemu ya mjadala huu wa kimataifa, iliitambua Palestina kabla ya kuibuka kwa mapigano ya Oktoba 7, 2023.
Umoja wa Afrika uliipa Palestina Hadhi ya Mtazamaji mwaka 2013 na kumruhusu kiongozi wake kuzungumza katika kila mkutano wa kila mwaka wa AU. Bendera ya Palestina inapepea pamoja na bendera nyingine za Afrika katika Tume ya Umoja wa Afrika nchini Ethiopia.
Palestina imethamini wimbi la kimataifa la kutambuliwa na kuliita ujumbe wa matumaini kwa watu wa Palestina, ujumbe wa matumaini kwa taifa huru. Israel kwa upande mwingine imesema wimbi hili linatishia kuwepo kwake.
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa litafanya kikao maalumu kujadili suala la Palestina na Gaza inasubiri kuona ikiwa ulimwengu itawapa heshima wanayostahili.