AFRIKA
2 dk kusoma
Jeshi la Nigeria limekanusha kukamatwa baadhi yao kwa 'njama ya mapinduzi' dhidi ya Tinubu
Taarifa ya awali ya jeshi ilisema maafisa 16 wamekamatwa kwa "maswala ya utovu wa nidhamu''.
Jeshi la Nigeria limekanusha kukamatwa baadhi yao kwa 'njama ya mapinduzi' dhidi ya Tinubu
Jeshi la Nigeria limekanusha kukamatwa maafisa kwa njama ya kupindua Tinubu. / Nigeria Presidency
tokea masaa 13

Mamlaka za Nigeria siku ya Jumamosi zilikanusha madai kwamba zaidi ya maafisa kumi na wawili walikamatwa kwa tuhuma za kupanga mapinduzi, zikikanusha ripoti za vyombo vya habari vya ndani.

Nchi hiyo ya Afrika Magharibi imepitia mapinduzi ya kijeshi mara kadhaa katika historia yake na ilitawaliwa na wanajeshi kwa muda mrefu wa karne ya 20 tangu ilipopata uhuru kutoka Uingereza mwaka 1960.

Mapinduzi mapya yangerudisha nyuma maendeleo ya zaidi ya miaka ishirini na tano ya demokrasia isiyokatizwa.

"Jeshi la Nigeria (AFN) linapenda kusema wazi kwamba madai yaliyochapishwa na chombo hicho cha habari si ya kweli kabisa," alisema Tukur Gusau, mkurugenzi wa habari za ulinzi, bila kutaja jina la chombo cha habari alichomaanisha.

Hata hivyo, Sahara Reporters, chapisho la mtandaoni, na Premium Times, lenye makao yake makuu Abuja, ziliripoti Jumamosi kwamba angalau maafisa 16 walikuwa wakipanga kumuondoa madarakani Rais Bola Tinubu, ambaye alichukua madaraka mwaka 2023 baada ya kushinda uchaguzi.

‘Uchunguzi wa ndani’

Jeshi lilitangaza mapema mwezi huu kwamba maafisa 16 walikamatwa kwa "masuala ya utovu wa nidhamu".

Vyombo hivyo viwili vya habari, vikirejelea vyanzo vya ulinzi, viliripoti kwamba kukamatwa huko kulihusiana na mpango wa mapinduzi.

Mapema mwezi huu, jeshi lilisema kwamba "zoezi la kawaida la kijeshi limesababisha kukamatwa kwa maafisa kumi na sita kwa masuala ya utovu wa nidhamu na ukiukaji wa kanuni za huduma."

Taarifa ya jeshi iliongeza: "Uchunguzi umebaini kuwa malalamiko yao yanatokana zaidi na kudumaa kwa maendeleo ya kazi kutokana na kushindwa mara kwa mara katika mitihani ya kupandishwa vyeo, miongoni mwa masuala mengine."

Katika taarifa ya Jumamosi, Gusau alisema uchunguzi huo ni "mchakato wa kawaida wa ndani unaolenga kuhakikisha nidhamu na taaluma vinadumishwa ndani ya safu za jeshi."

CHANZO:TRT Afrika and agencies